• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
MATHEKA: Polisi wanahitaji ushauri nasaha na mazingira bora

MATHEKA: Polisi wanahitaji ushauri nasaha na mazingira bora

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka mingi, maafisa wa polisi nchini wamekuwa wakifahamika kwa ukatili dhidi ya raia na ulaji hongo.

Ripoti za mashirika mbalimbali zimewalaumu kwa ukiukaji wa haki za raia.

Lakini sasa matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kuwa ukatili wa maafisa hao umechukua mkondo tofauti huku wakijitoa uhai, kuwaua wenzao na watu wa familia zao.

Katika kisa cha hivi punde, afisa mmoja katika kituo cha polisi cha Kamukunji Kaunti ya Nairobi, alimuua mwenzake na kisha akajiua.

Hii inaonyesha kuwa kuna matatizo ya ndani katika kikosi hicho yanayohitaji kutatuliwa kwa dharura iwapo polisi watatengemewa kuwalinda raia.

Ni vigumu kwa afisa wa polisi aliye na matatizo ya kikazi yanayomkosesha utulivu kudumisha usalama wa raia.

Kumekuwa na visa vya maafisa wa vyeo vya chini kulalamika kwamba wakubwa wao huwa wanawadhulumu.

Awali, kumekuwa na visa vya maafisa hao kuwashambulia na hata kuwaua wakubwa wao.

Haya ni baadhi ya matatizo yanayofaa kuchunguzwa na kutatuliwa lakini inaonekana maafisa wakuu wa polisi nchini huwa wanayapuuza.

Maafisa wa polisi huwa wanahudumu katika mazingira hatari na mangumu sana na wanahitaji ushauri nasaha kila wakati.

Haifai kumpatia likizo ya miezi mitatu afisa anayefyatuliana risasi na magaidi eneo la kaskazini mwa Kenya bila kushughulikia maslahi yake ya kisaikolojia.

Wakati mwingine maafisa hao huwa wanaenda likizo bila marupurupu ya kuwakimu kimaisha na familia zao na wanaporudi kazini wakiwa wameacha familia zao bila chochote, wakuu wao wanaanza kuwatisha badala ya kusikiliza kilio chao.

Hali kama hii inaweza kutumbukiza afisa wa polisi katika mfadhaiko. Baadhi yao, naam, wengi wao, wamekuwa wakizama katika ulevi wa kupindukia kwa kuathiriwa na mfadhaiko.

Inasikitisha kwamba wakuu wao vituoni, ambao ninaamini huwa wamefunzwa mbinu za usimamizi huwa hawawezi kutambua maafisa wao wanapokumbwa na matatizo ya akili hadi pale wanaposababisha maafa au kujiua.

Nashawishika kuamini kuwa mojawapo wa vyanzo vya matatizo yanayokumba maafisa wa polisi kiasi cha kuwasukuma kuua wenzao au wakumbwa wao ni mtaala wa mafunzo ambao unawakadamiza wale wa vyeo vya chini.

Baadhi ya maafisa wamekuwa wakilalamika kwamba yao ni kufuata amri ya wakumbwa wao na hawafai kuwapinga.

Kumekuwa na habari za wakubwa kupuuza malalamishi ya maafisa wanaohudumu chini yao.

Hii imefanya maafisa wengi wa polisi kukosa pa kukimbilia kutafuta msaada wanapotatizika na kubaki wakiteseka ndani kwa ndani.

Mateso hayo huuzaa hasira ambazo hudhihirika wanapoua wenzao na hata kujitia kitanzi.

Mtaala wa mafunzo ya polisi unawafanya kujitenga na raia wa kawaida kwa kujiona binadamu bora zaidi asiyefaa kupatwa na matatizo yanayowakumba watu wengine unafaa kurekebishwa.

Maafisa wakuu wa polisi kuanzia vituoni wanafaa kuwapa sikio wale wanaohudumu chini yao na zaidi ya yote wanafaa kukoma kuwakinga wanaohusika na visa vya ukatili dhidi ya umma.

Ili kutekeleza wajibu wao wa kudumisha usalama kikamilifu, maafisa wa polisi wanahitaji utulivu wa akili. Vikao vya ushauri nasaha vya pamoja na vya afisa binafsi na familia zao vinafaa kuhimizwa kila baada ya miezi sita au mwaka.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ilipaswa kuboresha shule

COVID-19: Walimu kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo...