• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
WANGARI: Serikali ibuni mbinu kabambe za kukusanya kodi nchini

WANGARI: Serikali ibuni mbinu kabambe za kukusanya kodi nchini

Na MARY WANGARI

SERIKALI inapoelekeza juhudi zake katika ufufuzi wa mifumo ya kiuchumi 2021, pana haja ya kuwepo njia za kibunifu kuhusiana na utozaji kodi ili kuepuka kuwaongezea walipa ushuru mzigo zaidi.

Likizo ya ulipaji kodi iliyotangazwa na serikali kufuatia janga la Covid-19, ilikamilika wiki iliyopita mnamo Disemba 31 hivyo kumaanisha kwamba wananchi sasa watalazimika kulipa kiasi zaidi cha kodi.

Wakati wa likizo hiyo, kodi inayotozwa mapato ya raia pamoja na mashirika mbali mbali ilipunguzwa kwa asilimia tano mtawalia huku ushuru unaotozwa bidhaa ukipunguzwa kwa asilimia mbili.

Hatua hiyo ya serikali ya kupunguza kodi ilikuwa afueni kuu kwa wananchi maadamu iliwawezesha kusalia na kiasi kikubwa zaidi cha fedha za matumizi zilizosambazwa katika shughuli za kiuchumi.

Huku 2021 ikiashiria matumaini tele kijamii, kiuchumi na kisiasa baada ya kipindi kigumu mwaka uliopita, ni dhahiri kwamba ni mwaka wenye shughuli tele ikiwemo kurejea kwa watoto wote shuleni nchini kufuatia likizo ya miezi tisa kutokana na gonjwa la virusi vya corona na kupanda kwa joto la kisiasa katika maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Yote hayo yakijiri ni muhimu kutilia maanani juhudi za kufufua tena sekta ya kiuchumi nchini iliyopata pigo kuu kutokana na athari za virusi vya corona.

Kando na kupatia kipaumbele suala la kuimarisha mifumo ya kiuchumi ni sharti serikali na wadau husika wabuni mbinu za kisasa zitakazoboresha ukusanyaji wa kodi kutoka kwa walipa ushuru.

Ni muhimu kuwezesha usawa kati ya kiwango cha ushuru kinachohitajika kukusanywa na serikali na kiwango cha kodi kinachotozwa raia binafsi na mashirika mbalimbali.

Kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini Kenya, ni bayana kwamba ni asilimia ndogo ya Wakenya wanaopata mshahara hivyo kumaanisha ni wachache tu wanaoweza kulipa kodi ya mapato.

Endapo serikali itafanikisha juhudi zake za kufufua uchumi, itakuwa vyema zaidi kutoza idadi kubwa ya Wakenya kiwango cha chini cha ushuru badala ya kuwatoza raia wachache kiwango cha juu kupindukia cha kodi.

Kwa kufanya hivyo, ni muhimu mno kujihadhari dhidi ya kulemaza wananchi na kodi mpya za ziada kiholela ambazo matokeo yake ni kuwafanya baadhi kutafuta mbinu za kukwepa kulipa ushuru hivyo kuhujumu mchakato wote.

Mchakato wa ukusanyaji kodi unapaswa kuwa na lengo jumuishi linalomshirikisha kila mlipa ushuru kwa matokeo bora na kuvutia imani ya raia kwamba ushuru wanaotozwa ni kwa maslahi ya maendeleo ya taifa kwa jumla.

Isitoshe, jinamizi la ufisadi linapaswa kukabiliwa kwa kila namna hasa ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa umma huishia mifukoni mwa viongozi wachache walafi hivyo kuwafanya raia kukosa maana ya kulipa ushuru.

Ni kweli serikali inahitaji kukusanya kodi kutoka kwa walipa ushuru ili kuendesha shughuli na huduma za umma.

Hata hivyo, kiwango cha ufanisi kiuchumi katika taifa hakitegemei kiasi kikubwa cha ushuru unaotozwa raia hali ambayo imethibitishwa na baadhi ya mataifa duniani yaliyostawi kiuchumi ilhali yanatoza kiwango cha chini cha ushuru.

Ili Kenya iweze kupiga hatua kiuchumi, ni sharti kuwepo mbinu za kibunifu kuhusu mchakato wote wa kukusanya kodi ambao kando na kuwaimarisha Wakenya kifedha, pia utawezesha kufanikisha maendeleo nchini bila kuwafanya kuwa maskini.

[email protected]

You can share this post!

Umeme Bees na mabingwa watetezi Kingstone FC wadenguliwa...

CAF: Kipi kitarajiwe mechi ya Gor Mahia dhidi ya CR...