• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Spurs wakomoa Brentford 2-0 na kufuzu kwa fainali ya Carabao Cup

Spurs wakomoa Brentford 2-0 na kufuzu kwa fainali ya Carabao Cup

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho aliwaongoza Tottenham Hotspur kupepeta Brentford 2-0 mnamo Jumanne na kutinga fainali ya Carabao Cup msimu huu wa 2020-21.

Moussa Sissoko aliwafunguliwa Spurs ukurasa wa mabao kunako dakika ya 12 kabla ya Son Heung-min kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao katika dakika ya 70.

Spurs kwa sasa watakutana na mshindi wa nusu-fainali ya pili itakayowakutanisha Manchester United na Manchester City ugani Old Trafford mnamo Januari 6, 2021. Mechi ya fainali imeratibiwa kutandazwa mnamo Jumapili ya Aprili 25, 2021 uwanjani Wembley, Uingereza.

Kwa mujibu wa vinara wa ligi ya soka ya Uingereza (EFL), maamuzi hayo ya kuahirisha fainali hiyo kutoka Jumapili ya Februari 28 yalichochewa na haja ya kutoa jukwaa la mahudhurio ya mashabiki wengi iwezekanavyo.

Hata hivyo, idadi ya mashabiki watakaokubaliwa kuhudhuria mchuano huo itategemea kanuni zitakazokuwa zimetolewa na Serikali ya Uingereza wakati huo kuhusiana na jinsi ya kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Wakivaana na Spurs, Ivan Toney alidhani alikuwa amesawazishia waajiri wake Brentford katika 66 kabla ya bao lake kufutiliwa mbali na refa aliyerejelea teknolojia ya video ya VAR na kubaini kwamba alikuwa ameotea.

Brentford walikamilisha mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 pekee ugani baada ya kiungo Josh Dasilva kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkabili kiungo mkabaji Pierre-Emile Hojbjerg katika dakika ya 84.

Spurs wanawinda taji lao la kwanza tangu 2008 na Mourinho amesisitiza kwamba ana kiu ya kushindia waajiri wake ufalme wa taji hilo.

Hata hivyo, amewataka masogora wake kutolegeza kamba wanapojifua kwa hatua ya fainali ya kivumbi hicho ikizingatiwa kwamba wapinzani wao Brentford watashuka dimbani kwa matarajio makuu ya kuwadengua.

Mourinho ni mshindi mara nne wa taji la Carabao Cup japo waajiri wake Tottenham hawajawahi kutia kibindoni ufalme wa kombe lolote tangu 2008.

Mkufunzi huyo raia wa Ureno ndiye kocha wa tatu kuwahi kutinga fainali ya Carabao Cup akidhibiti mikoba ya vikosi vitatu tofauti.

Mshindi wa kipute cha Carabao Cup msimu huu hatafuzu kwa Europa League kama ilivyokuwa awali.

Badala yake, atafuzu kwa gozi la Uefa Europa Conference League ambalo ni shindano jipya kwenye kalenda ya soka ya bara Ulaya.

Spurs waliwapiga Stoke City 3-1 mnamo Disemba 23 kwenye robo-fainali na kujikatia tiketi ya kusonga mbele kwenye Carabao Cup muhula huu.

Mechi ya Januari 5, 2020 ilikuwa ya kwanza kwa Brentford kukutana na Spurs tangu mwaka wa 2000.

Brentford walifuzu kwa hatua ya nne-bora ya Carabao Cup muhula huu baada ya kuchabanga Newcastle United 1-0 mnamo Disemba 22, 2020.

Man-United walifuzu kwa hatua ya nusu-fainali za Carabao Cup baada ya kutandika Everton 2-0 kwenye robo-fainali mnamo Disemba 23, 2020 uwanjani Goodison Park.

Kwa upande wao, Man-City walitinga hatua ya nusu-fainali za Carabao Cup baada ya kuponda Arsenal 4-1 kwenye robo-fainali na watashuka dimbani mnamo Januari 6 wakiwinda ushindi ambao unatarajiwa kuwazolea ubingwa wa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.

Man-City waliwacharaza Man-United kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye nusu-fainali za mikondo miwili ya Carabao Cup mnamo 2019-20.

Kinyume na misimu mingine ya awali ambapo michuano ya hatua ya nne-bora ya Carabao Cup imekuwa ikitandazwa nyumbani na ugenini, mechi za muhula huu zimekuwa za mkondo mmoja pekee ili kuepuka mrundiko wa mechi baada ya kampeni za msimu huu wa 2020-21 kuchelewa kuanza kwa sababu ya corona.

You can share this post!

Olunga pua na mdomo kuyoyomea Qatar kuvalia jezi za...

Manchester City kumsajili beki Sergio Ramos iwapo Real...