• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Visa 40 vya maambukizi ya Covid-19 vyaripotiwa miongoni mwa vikosi vya EPL

Visa 40 vya maambukizi ya Covid-19 vyaripotiwa miongoni mwa vikosi vya EPL

Na MASHIRIKA

VINARA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamethibitisha visa 40 vya maambukizi ya Covid-19 miongoni mwa maafisa na wanasoka wa vikosi mbalimbali baada ya kufanywa kwa vipimo vya afya wiki iliyopita.

Idadi hiyo ya maambukizi ni zaidi ya maradufu ya visa vilivyoripotiwa katika juma lililotangulia na ni matokeo ya kupimwa kwa sampuli 2,295.

Jumla ya mechi tatu za EPL ziliahirishwa wiki iliyopita baada ya visa vya maambukizi kuripotiwa kambini mwa Manchester City na Fulham.

Kati ya Disemba 28-31, 2020 kuliripotiwa visa 28 vya maambukizi ya corona na visa 12 zaidi vikaripotiwa kati ya Januari 1-3, 2021.

Awali, jumla ya visa 18 vya maambukizi vilikuwa vimeripotiwa kutokana na vipimo vilivyofanyika kati ya Disemba 21-27, 2020.

“Licha ya ongezeko la maambukizi, usimamizi wa EPL bado una imani kwamba vikosi vinavyoshiriki kivumbi hicho vitaendelea kuzingatia kanuni zote zilizopo katika juhudi za kudhibiti janga la corona,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na vinara wa soka ya Uingereza.

Ili kuepuka mrundiko wa mechi kwenye kalenda inayojumuisha kampeni za EPL, League Cup na Kombe la FA, wasimimizi wa Ligi Kuu ya Uingereza wameshikilia kwamba kampeni za vipute hivyo zitaendelea jinsi zilivyoratibiwa ili msimu huu ukamilike kabla ya fainali za Euro 2021 kuanza Juni 11.

Ongezeko la visa vya maambukizi ya corona miongoni mwa vikosi vya EPL limehusishwa na utovu wa nidhamu kati ya wanasoka wa klabu mbalimbali.

Picha za Erik Lamela, Sergio Reguilon na Giovani Lo Celso ambao ni wachezaji wa Tottenham Hotspur pamoja nay a Manuel Lanzini wa West Ham United zilisambazwa mitandaoni mnamo Disemba 25, 2020 baada ya wanne hao wakiandaa dhifa iliyohusisha familia zao na wageni waliojumuika nao katika siku ya Krismasi.

Man-City pia wameanza uchunguzi kuhusu kisa ambapo beki Benjamin Mendy aliandaa hafla iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali nyumbani kwake siku ya kukaribisha Mwaka Mpya wa 2021.

Licha ya kukiuka baadhi ya kanuni zinazodhibiti maambukizi ya Covid-19, Reguilon na Mendy walijumuishwa katika vikosi vya wanasoka wa akiba kambini mwa Tottenham na Man-City mtawalia mwishoni mwa wiki iliyopita.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume apata majeraha kwa kugongwa na gari Thika Road

Serikali yafunga shule yenye madarasa hatari Mukuru