• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wataalam watarajiwa China kuchunguza kiini cha corona

Wataalam watarajiwa China kuchunguza kiini cha corona

Na MASHIRIKA

BEIJING, China

WATAALAM wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wanatazamiwa kufika China kuchunguza kiini cha virusi vya corona, mwaka mmoja baada ya kuzuka kwa mkurupuko huo.

Ziara hiyo inaandamwa na siasa kali, shutuma za kuwepo njama fiche, usiri na hofu ya kasumba za magharibi.

Mbele ya ulimwengu wote Beijing ilichelewesha kuwaruhusu wataalam wasioegemea upande wowote kuingia China kuchunguza chanzo cha janga hilo la kiafya na kusitasita kufanyiwa uchunguzi.

WHO, sasa inasema China imetoa kibali cha ziara ya wataalam wake ambapo timu ya watu kumi inatarajiwa kuwasili hivi punde kwa ziara ya siku tano au sita – ikiwemo wiki mbili watakazokaa katika karantini.

Serikai ya China wiki hii ilikataa kuthibitisha tarehe halisi na maelezo ya kina kuhusu ziara hiyo, hatua iliyoashiria uzito wa shughuli hiyo.

Covid-19 iligunduliwa kwa mara ya kwanza katika eneo la kati la mji wa Wuhan mwishoni mwa 2019, kabla ya kuenea nje ya mipaka ya China na kuzua balaa kwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1.8 milioni kote ulimwenguni na kuzorotesha sekta za kiuchumi.

Kiini cha ugonjwa huo kimesalia mjadala mkali ambao umeibua lawama nyingi miongoni mwa jamii ya kimataifa pamoja na kutolewa kwa ripoti tatanishi na serikali ya China iliyopania kudhibiti usemi wake kuhusu virusi hivyo.

Timu ya WHO imeahidi kutilia maanani sayansi, hususan jinsi virusi hivyo vya corona vilivyoweza kuruka kutoka kwa wanyama – wanaoaminika kuwa popo – hadi kwa binadamu.

“Hii haihusu kupata taifa au serikali iliyo na hatia. Hii inahusu kuelewa kilichotendeka ili kuepuka hali kama hiyo siku za usoni na kupunguza athari,” alisema Fabian Leendertz kutoka Taasisi ya Robert Koch, Shirika Kuu la kudhibiti maradhi Ujerumani, ambaye atakuwa miongoni mwa wanasayansi watakaosafiri.

Ziara hiyo haitakuwa ya kwanza ambapo makundi yamezuru China kuhusiana na Covid-19.

Mwaka uliopita shughuli kama hiyo iliangazia hatua zilizochukuliwa na serikali za mataifa badala ya kiini cha virusi huku nyingine ikiandaa njia kwa uchunguzi unaosubiriwa.

Katika safari hii, WHO itajiweka katikati ya shutuma kutoka kwa mataifa ya magharibi na uongozi wa China uliopania kuonyesha kwamba mfumo wake wa kisiasa wenye usiri na michakato tele ulichangia kudhibiti na wala si kuenea kwa mkurupuko huo.

You can share this post!

Spika aliye mwiba kwa Trump kuongoza Congress muhula wa 4

Baadhi ya wazee wa jamii ya Talai ni wakora – Kinara