• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
KNPC yataja kikosi cha Riadha za Walemavu za Dubai Para Grand Prix

KNPC yataja kikosi cha Riadha za Walemavu za Dubai Para Grand Prix

Na AYUMBA AYODI

KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki (KNPC) imeteua jumla ya wanariadha 37, waelekezi 12 na maafisa 15 watakaowakilisha Kenya kwenye mashindano ya Riadha za Dubai Para Grand Prix mnamo Februari 7-14, 2021.

Wakati uo huo, KNPC imesema kwamba itahitaji kima cha Sh26 milioni ili kufanikisha mipango yao ya kushiriki kivumbi hicho cha Dubai ambacho kitakuwa sehemu ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan mwaka huu.

Kikosi cha Kenya kimefichuliwa baada ya kukamilika kwa mchujo ulioandaliwa katika uwanja wa MISC Kasarani.

Kwa mujibu wa Agnes Aluoch ambaye ni Rais wa KNPC, shirikisho lake tayari limeandikia Wizara ya Michezo kuhusiana na masuala ya ufadhili wa Sh26 milioni unaohitajika. Fedha hizo zitagharimia malaji, malazi na marupurupu ya wachezaji wakiwa katika kambi ya mazoezi kwa kipindi cha siku 10.

“Tunahitajika pia kununua kiti-maguru kimoja spesheli cha T54 pamoja na jezi za mashindano,” akasema Aluoch akiwa mwingi wa matumaini kwamba Serikali itazingatia ombi lao kwa wakati.

Ni matarajio ya Aluoch kwamba kikosi kitaingia kambini kuanzia Jumatatu ya Januari 11, 2021 ikizingatiwa kwamba mazoezi ya kutosha yatakuwa kiini cha kutamba kwa wachezaji wanaolenga pia kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo.

“Kuwaweka wachezaji kambini kutahakikisha kwamba hawaathiriwi na masuala yasiyostahili. Pia watakuwa na muda wa kutosha kufanya mazoezi ikizingatiwa kwamba corona ilivuruga mingi ya mipango ya mwaka uliopita wa 2020,” akasema Aluoch.

Kufikia sasa, Wakenya wanne wamefuzu kwa Olimpiki za Tokyo. Hao ni Nancy Chelagat, Hellen Wawira (powerlifting), Asia Mohammed (Para-rower) na Samwel Muchai aliyeibuka mshindi wa kitengo cha T11 kwenye Olimpiki za Walemavu za Rio 2016 katika mbio za mita 5,000.

“Idadi hiyo ya wachezaji huenda ikaongezeka ikizingatiwa wingi wa mashindano ya kufuzu kwa minajili ya fani mbalimbali. Isitoshe, tutapania kupata uwakilishi wa wachezaji ambao wameridhisha katika fani zao huku wakidhihirisha fomu nzuri kwa muda mrefu. Hivyo, kupata tiketi ya kufuzu pekee haitoshi kumwezesha mshindani kuelekea nchini Japan,” akasema Aluoch.

Licha ya kuwakilishwa na wanariadha tisa pekee kwenye Olimpiki za Walemavu za Rio mnamo 2016 nchini Brazil, Kenya ilijizolea jumla ya medali sita: tatu za dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba.

KIKOSI CHA KENYA:

WANAUME:

Wilson Bii (T11) 1,500m, 5,000m; Samwel Muchai (T11) 1,500m, 5,000m; Rodgers Kiprop (T11) 5,000m; Eric Sang (T11) 1,500m; John Torotich (T12) 1,500m, 5,000m; Bernard Koskei (T12) 1,500m, 5,000m; Henry Kirwa (T12) 1,500m, 5,000m; Samson Ojuka (T37) 100m, 200m, kuruka mbali; Gilbert Lagat (T12) 400m; Henry Nzungi (T12) 100m, kuruka mbali; Wesley Sang (T46) 1,500m, Stanley Misik (T46) 1,500m); Felix Kipruto (T46) 1,500m; Daniel Safari (F42) kuruka juu; James Magerere (F57) kurusha kijiwe, mkuki; James Mugo (F57) kurusha kijiwe, mkuki; Vincent Mutai (T46) 100m, kuruka mbali; Wilfred Laisikwa (T37) 200m, 400m; Ronald Yego (T37) 200m, 400m; Joseph Kamau (T37) 200m, 400m; Rajab Chetty (F11) kurusha kijiwe; Augustino Kilonzo (F11) kurusha kijiwe; John Njoroge (T11) 400m; John Wambua (T54), 100, 200m, 400m; Samson Njoroge (F57) kurusha kijiwe, mkuki; Joseph Kyaka (T 37) 1,500m.

WANAWAKE:

Nancy Koech (T11) 400m, 1,500m; Mary Waithera (T11) 400m, 1,500m; Nelly Nasimiyu (T12) 400m, 1,500m; Hannah Ngendo (T12) 400m, 1,500m; Irene Tanui (T46) 200m, 400m; Sylvia Olero (F44) kurusha kisahani; Nelly Sile (F56) kurusha kijiwe, mkuki; Margaret Njeri (F57) kurusha kijiwe, kisahani; Jennifer Chepkoech(f40) kurusha kijiwe; Linet Ogwal (F57) kurusha kijiwe, kisahani; Caroline Wanjira (T54) 100m, 200m, 400m.

Waelekezi: Robert Tarus, James Boit, Alpha Malinga, David Korir, Musa Muiruri, Kelly Otinya, Damaris Nzisa, Charles Macharia, Albanus Mutuku, Stephen Waweru.

TANBIHI:

T11- wasio na uwezo wa kuona kabisa; T12- walio na uwezo wa kuona kiasi; T37- walio na matatizo ya kupooza kwa ubongo; T46- waliokatwa mikono na miguu au walio na ulemavu wa ufupi wa mikono na miguu; T57- wanaorusha vijiwe na visahani wakiwa wameketi; F42- walio wafupi kupita kiasi; F44- wafupi walio na uwezo wa kurusha mikuki, visahani na vijiwe wakiwa wamesimama; T54- wanaoshiriki mbio wakiwa kwenye viti-maguru.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kocha Nuno Espirito wa Wolves atozwa faini ya Sh3.5 milioni...

Kikosi cha Apoel champiga kalamu kocha Mick McCarthy baada...