• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Sampdoria wapiga Inter Milan breki kali katika Ligi Kuu ya Italia

Sampdoria wapiga Inter Milan breki kali katika Ligi Kuu ya Italia

Na MASHIRIKA

ALEXIS Sanchez alipoteza penalti katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyoshuhudia Sampdoria wakiwanyuka 2-1 mnamo Januari 6, 2021.

Kichapo hicho ambacho Inter walipokezwa kilikomesha rekodi ya kutoshindwa kwao katika jumla ya mechi nane mfululizo za Serie A.

Chini ya kocha Antonio Conte, kikosi hicho kwa sasa kinajivunia alama 36, moja pekee nyuma ya viongozi wa jedwali, AC Milan walipepetwa 3-1 na Juventus kwenye mchuano mwingine wa Jumatano usiku katika soka ya Italia.

Antonio Candreva anayechezea Sampdoria kwa mkopo kutoka Inter alifunga bao la kwanza katika dakika ya 23 kupitia penalti kabla ya Keita Balde ambaye ni raia wa Senegal kupachika wavuni goli la pili kunako dakika ya 38.

Stefan de Vrij alirejesha Inter mchezoni katika dakika ya 65 baada ya penalti iliyochanjwa na Sanchez katika kipindi cha kwanza kupanguliwa na kipa Emil Audero.

Ashley Young alishuhudia fataki yake ikigonga mwamba wa goli la Sampdoria, jambo lililowahangaisha zaidi masogora wa Conte waliovurumisha makombora 24 langoni pa wenyeji wao.

Mechi hiyo ilishuhudia matukio matatu ambayo kikawaida yangezalisha penalti chini ya dakika 23 za kipindi cha kwanza. Tukio la kwanza lilifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR japo wanasoka wa Sampdoria walilalamika kwamba fowadi Lautaro Martinez alikuwa ameunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Tukio la pili lilizaa penalti iliyochanjwa na Sanchez baada ya kiungo Morten Thorsby kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. VAR ilibatilisha tena maamuzi ya refa aliyekuwa amewapa Sampdoria mkwaju wa penalti baada ya Nicolo Barella kudaiwa kuunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Mbali na Romelu Lukaku ambaye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Inter katika kampeni za Serie A kwa mabao 12 kufikia sasa, nyota mwingine aliyepoteza nafasi nyingi za wazi kwa upande wa kikosi cha kocha Conte ni Ivan Perisic.

Chini ya kocha Claudio Ranieri, ushindi wa Sampdoria ulikuwa wao wa kwanza baada ya miaka minne kusajili dhidi ya Inter katika ligi.

Kwingineko, AS Roma waliendeleza presha kwa washindani wao wakuu kileleni mwa jedwali la Serie A kwa kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Crotone wanaovuta mkia. Crotone waliingia uwanjani kwa minajili ya mchuano huo siku tatu baada ya kupokezwa kichapo kinono cha 6-1 kutoka kwa Inter.

Mabao ya Roma yalifumwa wavuni kupitia Henrikh Mkhitaryan na Borja Mayoral aliyecheka na nyavu za Crotone mara mbili.

Sassuolo walijinyanyua kutokana na kichapo cha 5-1 katika mechi ya awali dhidi ya Atalanta na kuwapiga Genoa 2-1. Bao la ushindi kwa upande wa Sassuolo lilijazwa kimiani na nyota Giacomo Raspadori katika dakika ya 83. Sassuolo kwa sasa wanajivunia alama 29 kutokana na mechi 16 ZA Serie A.

Ni pengo la pointi nne pekee ndilo linawatenganisha na Roma wanaofunga orodha ya tatu-bora kwa alama 33, nne nyuma ya viongozi wa jedwali AC Milan. Atalanta waliopepeta Parma 3-0 wanashikilia nafasi ya saba kwa alama 28 sawa na Napoli.

You can share this post!

Wanaraga wa Shujaa wapangiwa mechi zaidi za kirafiki barani...

BI TAIFA JANUARI 7, 2021