TAHARIRI: Serikali inatuficha nini huko shuleni?

KITENGO CHA UHARIRI

IWAPO kumewahi kuwa na mzaha wa kuchekesha zaidi ndani ya siku hizi saba za mwaka huu wa 2021, ni ule wa wizara ya Usalama wa Ndani na ile ya Elimu kuwapiga marufuku wanahabari shuleni.

Jumatano akiwa katika Kaunti ya Tharaka Nithi, waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i aliwazuia wanahabari kuandamana naye kwenye ziara yake.

Kitendo hicho kilijiri hata baada ya idara ya mawasiliano ya wizara zote mbili kuwatumia wanahabari mwaliko.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha akiwa Nairobi, alisingizia agizo la Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumapili, ambapo alisema watu wasiohusiana na mahitaji ya wanafunzi hawapaswi kuruhusiwa kuingia shuleni.

Siku ya Jumanne, Naibu Waziri wa Elimu Zack Kinuthia alisema kuwa lazima wanahabari wapate kibali kutoka kwa wizara hiyo ili kuingia katika shule yoyote na kupiga picha.

Serikali inadai kuwa uamuzi huo unalenga kuwapa wanafunzi, hasa watahiniwa wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne, muda wa kutosha kuendelea na masomo yao bila usumbufu wowote.

Prof Magoha anayewazuia wanahabari kufika shuleni, ndiye ambaye mwaka 2019 aliwarausha wanahabari na kwenda nao kwenye vituo ambako mitihani ilifungiwa. Kisha alifurahia kupigwa picha akizuru ndani ya madarasa ambamo watahiniwa walifanya mtihani huo.

Kutembelea shule sasa ambapo watahiniwa wanajiandaa, na kuingia chumba cha mtihani wakati watahiniwa wametaharuki, kipi ni usumbufu zaidi?

Wanachosahau mawaziri hawa ni kuwa, wanahabari pia ni wazazi. Baadhi yao huwapeleka shuleni watoto wao wadogo kila asubuhi.

Kutoa agizo kwamba wasiruhusiwe katika shule yoyote, ni ubaguzi na ukiukaji wa haki zao kama Wakenya. Wanahabari huingia hata maeneo yanayolindwa kama vile Ikulu ya Rais au kambi za Jeshi. Kuwazuia kuingia katika shule ni kutoielewa Katiba kuhusu haki ya umma kufahamishwa yanayoendelea.

Kama tulivyosema kwenye tahariri jana, serikali ilifeli katika maandalizi. Waziri Magoha alipoagiza watoto wasome hata chini ya miti, hakuwa ameenda Baringo na Nyando kutambua kuwa hata hiyo miti haiko.

Kuwazuia wanahabari sio tu kinyume cha sheria, bali ni ishara kuwa serikali inataka kuficha udhaifu wake, badala ya kuukabili kwa kuurekebisha.

Habari zinazohusiana na hii