• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
KAMAU: Kang’ata ni mwanga mpya tunaouhitaji hapa nchini

KAMAU: Kang’ata ni mwanga mpya tunaouhitaji hapa nchini

Na WANDERI KAMAU

TANGU zamani, fasiri kamili ya uzalendo huwa ni kuonyesha imani kwa kiongozi aliye mamlakani.

Ni hali ya kuridhika kuwa aliye uongozini atatekeleza na kutimiza matakwa ya wale waliomchagua.

Uwepo wa uzalendo kwa wale wanaoongozwa hujenga fahari nyoyoni mwao kuwa, nchi ama falme yao ndiyo bora zaidi kuliko zote.

Kijumla, uzalendo ndio huwawezesha wananchi kuendeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuwatii watawala na taasisi zilizopo bila tashwishi yoyote.

Ingawa huo ndio ufasiri ambao umekuwepo tangu uhuru, hasa miongoni mwa nchi zenye ukuaji wa kadri, maswali yanaibuka kuhusu ikiwa uzalendo unawazuia wale wanaoongozwa kuwauliza maswali viongozi wao.

Hili linafuatia hisia kali ambazo zimetolewa kuhusu hatua ya Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a, kumwambia Rais Uhuru Kenyatta kuwa huenda ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) isiungwe mkono kikamilifu katika ukanda wa Mlima Kenya.

Kwenye barua aliyomwandikia Rais Kenyatta mapema wiki hii, Dkt Kang’ata, ambaye pia ndiye Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, aliorodhesha masuala anayohisi yanapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya ripoti hiyo kuanza kuvumishwa katika eneo hilo na nchini kote.

Kufuatia uamuzi huo wa nadra, kuna wale wanaomsifu huku wengine wakimkosoa vikali kwa “kutomheshimu” Rais.

Kwa wale wanaosifia uamuzi wake, wanasema “ameonyesha ushujaa kumweleza Rais ukweli kuhusu hisia za wananchi.”

Nalo kundi ambalo limeeleza kutoridhishwa na hatua hiyo linamtaja kuwa kiongozi ambaye “hana hekima”, hasa baada ya kuiweka barua yake kuwa wazi.

Hisia hizo zote zinazua maswali kuhusu maana halisi ya uzalendo: Je, ni vibaya kwa kiongozi aliye mamlakani kukosolewa na viongozi wenzake? Je, ni kumkosea hekima kumkosoa kiongozi huyo? Wanaomkosoa wanapaswa kuadhibiwa?

Bila shaka, hayo ni maswali mazito yanayopaswa kutumiwa kama kigezo cha kuzua mdahalo pevu kuhusu maana halisi ya uzalendo, hasa katika jamii inayodai kuzingatia mfumo wa demokrasia kwenye utawala wake.

Tangu mfumo huo ulipoanza nchini Ugiriki karne nyingi zilizopita, waanzilishi wake walishikilia kuwa hauna ukamilifu ikiwa walio mamlakani hawawezi kuulizwa maswali kuhusu namna wanavyoziendesha jamii husika.

Kulingana nao, ukamilifu wa demokrasia ni pale ambapo viongozi wanawapa raia nafasi kuwauliza maswali, ili kubuni mazingira ambapo hawahisi kutengwa na uongozi uliopo.

Ni kutokana na mantiki hiyo ambapo nchi kama Amerika zimebuni utaratibu ambapo lazima wale wanaowania urais washiriki kwenye midahalo miwili pevu, kuwaeleza raia kuhusu mipango walio nayo kuhusu uongozi wa taifa hilo.

Vivyo hivyo, Kenya kamwe haiwezi kudai kuzingatia mfumo wa demokrasia na kuwanyamazia viongozi walio mamlakani. Maana halisi ya demokrasia ni wakati wanapoulizwa maswali na wanachukua nafasi yao kuyajibu.

Huo ndio uzalendo na uwajibikaji wa kweli.

Hivyo, Dkt Kang’ata hajakosea hata kidogo. Hajamnyima Rais Kenyatta heshima wala kuikosea nchi uzalendo.

Badala yake, amezingatia uhalisia kamili kuhusu demokrasia: kuuliza maswali. Badala ya kumkashifu, anapaswa kuwa mwanga mpya kwa Wakenya wote.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali inatuficha nini huko shuleni?

KING’ORI: Wapwani waunde chama kutetea maslahi yao...