• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
KING’ORI: Wapwani waunde chama kutetea maslahi yao vilivyo

KING’ORI: Wapwani waunde chama kutetea maslahi yao vilivyo

Na KINYUA BIN KING’ORI

VIONGOZI wa Pwani wanafaa kuwa wajasiri na kutangaza sasa kuunda chama kitakachowakilisha matakwa ya Wapwani.

Viongozi hao wanastahili kuchukua hatua hiyo iwapo wanataka kujumuishwa katika siasa za kitaifa na kuhusishwa katika maamuzi muhimu ya kisiasa na kiuchumi.

Inasikitisha kuwa wakati jamii zingine zinaendelea kusuka mikakati ya kujipanga kisiasa kabla ya 2022, viongozi wa Pwani wanaendelea kulumbana na kutengana huku wakiwa mashabiki sugu wa vyama visivyowahusu.

Mpwani anafaa kutambua ku ikiwa eneo halitakuwa na chama kinachowaakilisha ifikapo 2022, watakumbana na wakati mgumu mno kupata nafasi ya sauti ya Mpwani kuwakilishwa katika meza ya maamuzi kitaifa.

Baadhi ya wabunge wa Pwani akiwemo mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa walifurushwa ODM kwa hali zilizoonekana kuwa maonevu makuu, lakini hata baada ya hayo, viongozi hao hawajaonyesha juhudi zozote kuwa wanaweza kuungana na kuimarisha nyota yao kisiasa kwa kuwa na chama chao.

Hali hii pia inamaanisha kuwa, huenda 2022 wakadandia vyama visivyowahusu kwa njia yoyote.

Ushindi wa mbunge mpya wa Msambweni, Bw Feisal Abdallah aliyepata kura 15,251 na kumbwaga mgombea wa ODM, Bw Omar Boga aliyepata kura 10,444, na ambaye alikuwa amebashiriwa kushinda uchaguzi huo mdogo, ni ishara tosha Mpwani amezinduka.

Gavana wa Mombasa, Bw Hasan Joho na mwenzake wa Kwale, Bw Salim Mvurya, hawafai kuhadaika kukubali kutumiwa kuzua uhasama kisiasa na badala yake waungane kuhakikisha Mpwani atatimiza ndoto yake ya kuwa na chama kitakachowafaidi kisiasa kabla ya 2022.

Uchaguzi mkuu unapokaribia, miungano mipya ya kisiasa itachipuka baadhi ikidumishwa na kile Mpwani anatarajia kusikia ni miungano ikifanywa baina ya chama kinachowakilisha matakwa yake katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kielimu na kijamii.

Itakuwa vyema kuhakikisha kuwa wanachangamka kisiasa ili iwapo watakosa nafasi ya urais, angalau wananufaika kwa nafasi ya naibu.

Wapwani wanastahili kufahamu kuwa wakati ni sasa ambapo wanasstahili kujitokeza na kuhakikisha kuwa sauti yao inapazwa maamuzi muhimu ya kitaifa yanapofanywa.

Viongozi wote wa eneo hili wanafaa kutambua kuwa iwapo 2022 itafika kabla ya wao kuunda chama chao, basi watakumbana na wakati mgumu kujieleza kwa wakazi ambao wamechoka kutumikwa na wengine kuwapiga jeki kisiasa na kuwainua kiuchumi.

You can share this post!

KAMAU: Kang’ata ni mwanga mpya tunaouhitaji hapa nchini

Biden ampa Trump kichapo cha mwisho kura za useneta