• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Uwanja wa Nyayo kuwa mwenyeji wa duru zote tatu za Mbio za Kupokezana Vijiti za AK

Uwanja wa Nyayo kuwa mwenyeji wa duru zote tatu za Mbio za Kupokezana Vijiti za AK

Na CHRIS ADUNGO

DURU zote tatu za Mbio za Kupokezana Vijiti za Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) zitaandaliwa katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mashindano wa AK, Paul Mutwii, imekuwa vigumu kwa shirikisho kuandaa mapambano ya haiba kubwa nje ya Nairobi kwa sababu ya changamoto tele za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Awali, Nairobi ilitarajiwa kuwa mwenyeji wa duru ya kwanza mnamo Januari 9, 2021, huku duru ya pili ikitarajiwa kufanyika katika eneo la North Rift mnamo Januari 23.

Uwanja wa Kericho Green ulikuwa uwe mwenyeji wa duru ya tatu mnamo Februari 6 kabla ya mchujo wa kitaifa kwa minajili ya kufuzu kwa Mbio za Dunia za Kupokezaka Vijiti kufanyika kati ya Machi 26-27 ugani Nyayo.

Mbio za Dunia za Kupokezana Vijiti zimeratibiwa kufanyika mjini Selesia, Poland mnamo Mei 1-2, 2021.

“Kwa sababu ya kanuni za usafiri na masharti mengine yaliyopo katika vita vya kudhibiti janga la corona, AK imeamua kwamba duru zote tatu za mbio za kupokezana vijiti zifanyike ugani Nyayo, Nairobi,” akasema Mutwii kwa kushikilia kwamba tarehe za kuandaliwa kwa kila duru zitasalia jinsi ilivyokuwa awali.

Hata hivyo, kinara huyo alifichua kwamba kutakuwa na mabadiliko katika jinsi ambavyo mbio za kawaida za masafa mafupi na kadri katika fani hiyo zimekuwa zikifanyika.

Wanariadha kwa sasa watalazimika kushindana katika mita 150, mita 300, mita 500, mita 100 kuruka viunzi, mita 1,000 na mita 1,500.

Aidha, kutakuwepo na fani nyingine ya mbio za kupokezana vijiti za 4x200m na 4x400m mseto (wanaume na wanawake).

Wanariadha watarejea katika mfumo na kukimbia umbali wa kawaida kwenye fani ya mbio hizo kwenye duru ya pili na tatu.

Mutwii amesisitiza kwamba watakaoshiriki duru ya tatu watakuwa waalikwa pekee ambao watakuwa wameteuliwa tayari kutokana na ubora wa matokeo yao katika duru ya kwanza na pili.

“Mwanariadha yeyote ambaye hatashiriki duru ya kwanza na pili hatakubaliwa kunogesha duru ya tatu na mchujo wa kitaifa,” akaonya Mutwii.

Fani zitakazoshirikishwa kwenye Mbio za Dunia za Kupokezana Vijiti ni 4x100m, 4x200m, 4x400m, 4x400m mseto (wanaume na wanawake), 2x2x400m na 1x400m kuruka viunzi (wanaume na wanawake).

You can share this post!

Polisi wachunguza kisa cha mwanamume kuzirai na kufariki...

Waboni walilia serikali watoto wapate elimu