Ruto ataka Raila abebe ‘dhambi’ kadhaa za Jubilee

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto anataka kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga akome kujitenga na changamoto zinazokumba taifa wakati wa utawala wa serikali ya Jubilee.

Naibu wa Rais alisema kuwa tangu Rais Uhuru Kenyatta aingie mwafaka na Bw Odinga mwaka wa 2018, kiongozi wa nchi amekuwa akiwasikiliza na kupokea ushauri kutoka kwa viongozi wa upinzani.

Hivyo basi, alimtaka Bw Odinga pamoja na vigogo wengine wa kisiasa wasitoroke wakati serikali inapolaumiwa, bali washirikiane kutatua changamoto zilizopo.

“Handisheki imefanya mambo kuwa rahisi sana kwani viongozi wote tunatangamana na kuzungumza. Viongozi wa muungano wa NASA ambao walikuwa wapinzani wetu sasa wana nafasi sawa na mimi ya kukutana na kushauriana na Rais.

“Bw Musalia, Seneta Moses Wetangula, Bw Kalonzo Musyoka na Agwambo (Bw Odinga) –wote wanazungumza na rais na kuzikilizwa. Hivyo msiwe na sisi wakati wa raha na kisha kutuhepa changamoto zinapojitokeza. Tuungane na tukabiliane na changamoto zilizosababishwa na janga la virusi vya corona kama vile kudorora kwa uchumi,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais alikuwa akizungumza wakati wa ibada ya kumuaga Bi Hannah Mudavadi – mamaye kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi – katika Kanisa la Friends International Centre Church (Quakers), mtaani Ngong, Nairobi.

Dkt Ruto alisema hayo siku chache baada ya Bw Odinga kumtaka kutokwepa ‘maovu’ yaliyofanywa na serikali ya Jubilee.

Bw Odinga alipokutana na wasomi wa Kiislamu jijini Mombasa wiki iliyopita, alimshutumu Dkt Ruto kwa kujaribu kukwepa makosa

“Raila hajaingia serikalini. Mimi ninatekeleza tu yale tuliyokubaliana na Rais Kenyatta. Lakini yule (Naibu wa Rais Ruto) ambaye amekuwa na Rais kwa miaka minane sasa anaruka eti hafai kuwajibikia makosa yaliyotekelezwa na serikali ya Jubilee.

“Yeye (Ruto) anapokea mshahara, amepewa maafisa wa usalama wa serikali na amepewa kila kitu kama naibu wa rais; halafu sasa anaanza kuhujumu hiyo serikali kwa kusema kuwa Raila ndiye anafaa kuwajibika,” akasema Bw Odinga.

Lakini Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, Alhamisi alisisitiza kuwa chama cha ODM kinafaa kuchukua sehemu ya lawama kutokana na makosa ambayo yamefanywa na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na Bw Cherargei, utendakazi duni wa serikali ya Jubilee utamfanya Bw Odinga kukataliwa na Wakenya endapo ataamua kuwania urais 2022.

“Handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga itasambaratika hivi karibuni. Chama cha ODM tayari kimebaini kuwa utendakazi wa serikali ya Jubilee ni duni. Wanajua kuwa wakiendelea kuwa na uhusiano na Jubilee wataadhibiwa na Wakenya katika uchaguzi mkuu ujao. Sasa wameanza kujitenga na makosa ya Jubilee,” Seneta Cherargei akaambia kituo kimoja cha runinga cha humu nchini.

Bw Cherargei pia alidai kuwa Rais Kenyatta ameanza kukwepa Mpango wa Maridhiano (BBI) baada ya kubaini kuwa kuna mambo muhimu ya kitaifa yanayofaa kupewa kipaumbele na kushughulikiwa kwa dharura kama vile ufufuaji wa uchumi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Ruto amhepa Uhuru

Wababaisha ‘Baba’