• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
Waboni walilia serikali watoto wapate elimu

Waboni walilia serikali watoto wapate elimu

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa jamii ya Waboni wanaoishi vijiji vilivyo msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, sasa wanaitaka serikali kubuni kituo maalum cha elimu kwenye kijiji cha Kiangwe ili kuwawezesha watoto kutoka jamii hiyo kusoma wakiwa mahali pamoja.

Wakazi hao wametoa pendekezo hilo baada ya shule sita zilizoko eneo hilo kukosa kufunguliwa walimu wanaozihudumia walipokosa kufika shuleni wakihofia kushambuliwa na magaidi.

Shule ambazo bado hazijafunguliwa ni Bodhai, Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe, hali ambayo imefanya wanafunzi zaidi ya 400 kusalia nyumbani.

Walimu walikataa kusafiri kwa barabara kwa kuhofia kushambuliwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.

Hata hivyo, majadiliano kati ya afisi ya elimu na idara ya usalama eneo la Lamu yanaendelea ili walimu hao wasafirishwe kwa ndege hadi shuleni wakati wowote.

Katika kikao na wanahabari jana, viongozi na wazee wa jamii ya Waboni waliirai serikali kujenga shule ya bweni mjini Kiangwe ambayo itakuwa kituo cha elimu kitakachohudumia watoto wote wa vijiji vya msitu wa Boni.

Diwani wa Wadi ya Basuba, Bw Barissa Deko, alisema kukosa kufunguliwa kwa shule za msitu wa Boni kila mara kumeongeza idadi ya vijana wanaoacha masomo na kurandaranda mitaani kiholela.

Bw Deko alisema suluhu ya pekee itakayohakikisha wanafunzi kutoka jamii ya Waboni wanabaki shuleni kusoma kama wengine ni kuanzishwa kwa kituo hicho cha elimu.

Alisema kituo hicho kitafaa zaidi kuanzishwa katika kijiji cha Kiangwe ni bora zaidi cha kuanzisha kituo hich kwa sababu kinaweza kufikiwa kwa urahisi na watu wote ikilinganishwa na vijiji vingine vilivyoko msitu wa Boni.

“Tangu 2014, shule zetu hazijaweza kuhudumia watoto wetu inavyostahili. Mahangaiko ya Al-Shabaab yamesukuma shule zetu kufungwa kila mara, hivyo kuachia wazazi mzigo wa kukaa na wanafunzi vijijini,” akasema Bw Deko.

Alieleza kuwa, licha ya usalama kuimarishwa msituni Boni, walimu bado wamekuwa wakighairi kufundisha vijijini na hivyo shule zimesalia kufungwa.

“Hili limeongeza idadi ya watoto wanaoacha shule miongoni mwa Waboni. Tungeomba kituo cha pamoja cha elimu kubuniwa mjini Kiangwe. Walimu wote wapelekwe kwenye kituo hicho kitakachokuwa cha bweni na ambacho kitapewa ulinzi mkali saa zote. Wakifanya hivyo tunaamini watoto wetu watasoma na kuhitimu kama wengine,” akasema Bw Deko.

Kwa upande wake, Bw Abdallah Wakati alisema ukosefu wa elimu miongoni mwa Waboni huenda ukazuia jamii hiyo kupata ajira katika Bandari ya Lamu (Lapsset).

Bw Wakati aliioomba serikali kutafuta suluhu ya kudumu, ikiwemo kubuni kituo hicho cha pamoja cha elimu eneo lao ili watoto wao wapate elimu na kufaidi ajira mbalimbali nchini.

You can share this post!

Uwanja wa Nyayo kuwa mwenyeji wa duru zote tatu za Mbio za...

WHO yazuiwa kuingia China kuchunguza kiini cha Covid-19