UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina mbalimbali za malipo na dhima yake katika jamii

Na MARY WANGARI

TUMEKUWA tukiangazia aina mbalimbali ya malipo yanayotumika katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Hii leo tutaendeleza mada hiyo kwa kuangazia na kuchambua kwa kina ada hizo mbalimbali jinsi ifuatavyo:

Mahari – Ni malipo yanayotolewa ili kuoa mwanamke au kuolewa na mwanamme kuambatana na jamii husika.

Mwago – Ni malipo kwa mke wa kwanza yanayotolewa na mume anapomletea mke mwenza au ukipenda anapooa mke wa pili.

Tapisho – Haya ni malipo yanayotolewa kwa ngariba kwa ajili ya utahirishaji.

Fichuo – Haya ni malipo au zawadi anayopatiwa mvulana anapotoka jandoni.

Kudu – Haya ni malipo yanayolipwa na mwari kwa nyakanga wake kama adhabu kwa kukosa adabu akiwa unyagoni.

Ridhaa – Haya ni malipo anayopatiwa mtu aliyevunjiwa heshima au hadhi yake.

Hongo, rushwa, chirimiri,mvugulio, kadhongo, chauchau, kilemba – Haya ni malipo au zawadi anayotoa mtu ili kupata kwa njia haramu kitu au huduma asiyostahili.

Arshi au Dia – Haya ni malipo anayopatiwa mtu anayejitolea kutolewa damu.

Kilemba – Hii ni ada, malipo au zawadi za harusi wanazopatiwa wajomba wake bibiharusi. Pia ni malipo yanayotolewa na mwanafunzi kwa mhunzi wake baada kuhitimu mafunzo yake.

Bakora – Ni zawadi anayotoa mzazi kwa fundi akitaka mtoto wake afundishwe ufundi.

Mrabaha – Haya ni malipo anayopatiwa mwandishi na kampuni iliyochapisha kazi yake kila baada ya muda fulani wa mauzo. Pia ni pato au faida inayotokana na biashara.

Mchango – Ni malipo anayotoa mtu kwa hiari kwa mtu anayehitaji au kwa kufanya shughuli fulani kama vile kugharamia bili ya hospitali, ujenzi wa shule na kadhalika.

Fungule – haya ni malipo yanayotolewa kwa daktari.

Bahashishi – Hii ni zawadi anayopatiwa mtu kwa huduma bora, utumishi au kazi aliyofanya.

Kombozi au kiokozi – Haya ni malipo yanayotolewa kukombolewa kitu au mtu aliyetekwa nyara.

Urithi au urathi – Hii ni mali inayoachwa na marehemu na kupatiwa mtu fulani kama vile mtoto au mke wa marehemu.

Rehani – Haya ni malipo ya kitu kilichowekwa dhamana ili kikombolewe baadaye.

Kodi au pango – Hii ni ada au malipo ya nyumba au chumba kilichokodishwa yanayolipwa kila mwezi au baada ya kila muda na mpangaji kwa mpangishaji.

Honoraria – Haya ni malipo au kiasi fulani cha pesa anazolipwa mtu kama bakshishi kwa kazi maalum aliyofanya.

Bakshishi – malipo ya kuonyesha shukrani.

Thawabu – Haya ni malipo anayopata mtu kutoka Maulana kwa sababu ya kutii amri zake na kwa mema aliyofanya.

Rada – haya ni malipo kutoka kwa Maulani kama adhabu kwa mtu kw maovu aliyofanya.

Mapoza – Ni malipo anayopatiwa mtu aliyekwazwa ili kuondoa hasira yake.

Haka – Ni malipo yanayotolewa na jamaa kwa familia yake ili kufidia kosa alilotenda.

Natija, tija au faida – Hizi ni pesa za ziada anazopata mfanyabiashara.

Posho, marupurupu – haya ni malipo ya ziada anayopata mfanyakazi zaidi ya mshahara au ujira wke wa kawaida.

Karisaji – Ni malipo au ada ya muda uliopita.

Kiangazamacho, kiokozi, chorombozi, machorombozi, utotole – Ni zawadi au malipo anayopatiwa mtu kwa kugundua kitu au kushuhudia jambo fulani likitendwa wakati fulani.

Fola – Haya ni malipo au zawadi inayotolewa ili kumshika mtoto mchanga kwa mara ya kwanza.

Ukonavi, kipamkono, kipakasa au jazua – Haya ni malipo au zawadi anayopatiwa biharusi anapoonwa kwa mara ya kwanza.

Kikunjajamvi – Hii ni ada inayoweza kuwa pesa taslimu au mifugo wanayotozwa wafanyabiashara au wakazi wa mabaraza ya kizamani na ya kiasili.

Mukafaa – Ni malipo ya mshahara kwa mfanyakazi kutokana na faida iliyopatikana.

Mbiru – Haya ni malipo yanayotolewa kwa serikali kutokana na mishahara ya wafanyakazi wake.

Zaka au fungu la kumi – Hii ni asilimia kumi inayotolewa na waumini kutoka kwa mapato yao kama ishara ya shukrani kwa Mola.

Fungule – Haya ni malipo ya kwanza yanayotolewa kwa mganga au mpiga ramli.

marya.wangari@gmail.com

Habari zinazohusiana na hii