Malkia Strikers kupiga kambi ya mazoezi bara Asia au Ulaya kabla ya kutua Japan kwa Olimpiki

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya voliboli ya wanawake, Malkia Strikers, wamepangiwa kupiga kambi barani Ulaya au Asia kabla ya kuelekea jijini Tokyo, Japan kwa Michezo ya Olimpiki mnamo Julai 2021.

Kocha Paul Bitok ambaye anakinoa kikosi hicho amesema Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) linajadiliana na Slovenia, Uturuki na Japan kwa matarajio ya kwamba Malkia Strikers watapata fursa ya kushiriki mazoezi katika mojawapo ya mataifa hayo.

Kocha huyo amesisitiza kuwa ziara ya Malkia Strikers itathibitishwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

“Kambi hizo za ughaibuni zitakuwa za manufaa sana kwa Malkia Strikers ambao watapata fursa ya kupimana nguvu na baadhi ya vikosi vya haiba kubwa. Mbali na kuwapa wachezaji motisha, michuano hiyo ya kirafiki itakuwa jukwaa zuri kwa kikosi kupata tajriba na uzoefu wa kutosha katika ulingo wa voliboli ya kimataifa,” akasema.

Wachezaji wa Malkia Strikers wanatarajiwa kurejelea mazoezi mwezi huu chini ya uzingativu wa kanuni zote zinazopania kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Tuna ulazima wa kuanza mazoezi hivi karibuni ikizingatiwa kwamba hatuna muda wa kutosha baada ya kupoteza mwaka mzima wa 2020,” akasema Bitok katika kauli iliyoungwa mkono na Rais wa KVF, Waithaka Kioni.

Kabla ya kufunga safari hiyo, idadi kubwa ya wachezaji wa Malkia Strikers watakuwa na fursa ya kuwakilisha klabu zao katika mapambano ya Klabu Bingwa Afrika mnamo Machi. Bitok amekiri kwamba mashindano hayo yatakuwa fursa ya wanavoliboli hao kujifua hata zaidi kabla ya kutua Japan.

Wakiwa jijini Tokyo, Malkia Strikers watavaana na Serbia, Brazil, Korea Kusini, Jamhuri ya Dominican na wenyeji Japan ambao wametiwa nao katika Kundi A. Hiyo itakuwa mara ya tatu kwa Malkia Strikers kunogesha kampeni za Olimpiki.

Serbia waliojizolea medali ya fedha kwenye Olimpiki za Rio nchini Brazil mnamo 2016, ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia na bara Ulaya huku Brazil wakijivunia nishani ya dhahabu kutokana na makala mawili yaliyopita ya Michezo ya Olimpiki.

Miongoni mwa mashindano ya Shirikisho la Voliboli la Afrika (CAVB) ambayo wachezaji wa Malkia Strikers watashiriki pia mwaka huu ni Kombe la Afrika kwa chipukizi (wavulana kwa wasichana), Klabu Bingwa Afrika (wanaume na wanawake), mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 na Kombe la Afrika kwa watu wazima (wanaume na wanawake).

Kufikia sasa, Uganda wamethibitisha kuwa wenyeji wa Kombe la Afrika kwa wasichana chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 huku Nigeria wakipata idhini ya kuandaa mashindano ya wasichana chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18. Mashindano hayo yataandaliwa kati ya Januari 26 na Februari 7, 2021.

Tunisia itaandaa fainali za Kombe la Afrika kwa wavulana chipukizi wasiozidi umri wa miaka 19 kati ya Februari 1-6 huku Misri ikiwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Afrika kwa chipukizi wa kiume wasiozidi umri wa miaka 21 kati ya Februari 18-26.

Kabla ya kuanza kushiriki mechi za voliboli ya kimataifa, wachezaji wa humu nchini wamepangiwa kuanza kampeni za Ligi Kuu ya KVF mnamo Januari 23 huku vikosi vinane vya wanawake na 13 vya wanawake vikithibitisha kushiriki kivumbi hicho.

Vikosi vya wanawake ambavyo vimethibitisha ushiriki wao ligini kufikia sasa ni Kenya Defence Forces, Kenya Army, Kenya Prisons, Directorate of Criminal Investigations (DCI), Prison Nairobi, Nairobi Water, KCB na Kenya Pipeline.

Upande wa wanaume unawakilishwa na Forest Rangers, Kenya Prisons, Prisons Nairobi, Western Rangers, Equity, Rift Valley Prison, Vihiga, Kenya Army, Administration Police, Kenya Ports Authority, Prisons Mombasa, KDF na mabingwa watetezi, GSU.