Mkimbiaji nyota Kishoyian alenga juu 2021, atavizia rekodi ya kitaifa iliyodumu miaka 29

Na GEOFFREY ANENE

ALPHAS Leken Kishoyian amejiwekea malengo makubwa ya mwaka 2021.

Mkenya huyu ambaye anajivunia kuwa wa pili kwa kasi ya juu katika mbio za mita 400 nchini, anasema anataka kuwa mmoja wa watakaopeperusha bendera katika Riadha za Dunia za Kupokezana vijiti mjini Silesia, Poland mwezi Mei na katika Michezo ya Olimpiki mjini Tokyo, Japan (Julai/Agosti) pamoja na kuvizia rekodi ya kitaifa iliyowekwa na Samson Kitur miaka 29 iliyopita.

Mtimkaji huyu wa mbio fupi, ambaye amesema hatashiriki duru ya ufunguzi ya mbio za kupokezana vijiti ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) hapo Januari 9 uwanjani Nyayo, si mgeni katika Riadha za Dunia za kupokezana vijiti. Alishiriki makala mawili ya kwanza yaliyofanyika mjini Nassau, Bahamas mwaka 2015 na 2017 na pia alikuwa katika makala ya tatu mjini Yokohama, Japan (2019).

Aliwakilisha Kenya katika mbio za kupokezana vijiti za Afrika za Chipukizi (2011), Olimpiki jijini London, Uingereza (2012) na Rio de Janeiro, Brazil (2016), Riadha za Dunia mjini Moscow, Urusi (2013), Riadha za Afrika mjini Durban, Afrika Kusini (2016) na Asaba, Nigeria (2018) pamoja na Michezo ya Afrika mjini Rabat, Morocco (2019). Alikuwa katika timu iliyozoa medali ya dhahabu ya mbio za mita 4×400 kupokezana vijiti mjini Asaba.

“Nataka kuacha historia katika mbio za mita 400 kabla ya kujitosa katika mbio za mita 800. Najua naweza kutimiza ndoto hiyo nikivunja rekodi ya kitaifa. Ni mojawapo ya malengo nimejiwekea mwaka huu wa 2021,” alisema Kishoyian.

Atalazimika kufanya kazi ya ziada kufuta rekodi ya Kitur ya sekunde 44.18 ambayo imedumu miaka 29. Kishoyian alikaribia kuvunja rekodi hiyo Julai mwaka 2015 alipokamilisha mbio hizo za mzunguko mmoja kwa sekunde 44.75 jijini Nairobi. Anasema analenga kukamilisha umbali huo wa mita 400 kwa sekunde 44:10.

Kabla ya Kitur kuaga dunia Aprili 2003, aliweka rekodi hiyo katika nusu-fainali ya Olimpiki za Barcelona Nchini Uhispania mnamo Agosti 3, 1992. Kitur aliishia kuzoa nishani ya shaba mjini Barcelona alipokamilisha fainali kwa sekunde 44.24, huku Waamerika Quincy Watts (43.50) na Steve Lewis (44.21) wakifagia nafasi mbili za kwanza.

Kishoyian, ambaye mbio zake za mwisho zilikuwa Riadha za Continental Tour za Kip Keino Classic mjini Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020 alizokamilisha kwa sekunde 47.12 katika nafasi ya sita kati ya washiriki wanane, hakusitisha mazoezi yake wakati Kenya ilithibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya corona mnamo Machi 12 mwaka uliopita. Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko yote Machi 16, 2020 baada ya visa vya maambukizi kuongezeka kabla ya kutangaza kurejea kwa michezo kadhaa isiyo hatari ikiwemo riadha mwezi Septemba.

“Niliendelea na mazoezi kivyangu baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko. Sitashiriki duru ya kwanza ya mbio za AK za kupokezana vijiti, lakini nitakuwepo katika ya pili. Niko tayari kwa mashindano ya kupokezana vijiti ya AK,” alisema mkimbiaji huyo kutoka Idara ya Majeshi.

Hapo Januari 6, 2021, AK ilitangaza ratiba yake ya mbio za kupokezana vijiti zitakazofanyika uwanjani Nyayo mnamo Januari 9, Januari 23 na Februari 6 kabla ya mchujo wa kitaifa wa Riadha za Dunia za kupokezana vijiti mnamo Machi 26-27.