Wakenya wengi hawataki BBI – Utafiti

Na VALENTINE OBARA

UWEZO wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, kufanikisha safari ya urekebishaji katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), unazidi kugubikwa na shaka kadri na jinsi muda unavyosonga.

Utafiti sasa umeonyesha kuwa, endapo kura ya maamuzi itaandaliwa hii leo, hakutakuwa na marekebisho ya katiba kwani idadi kubwa ya Wakenya watakataa marekebisho hayo.

Ripoti ya utafiti huo uliofanywa na shirika la Tifa, ilitolewa Ijumaa, siku chache baada ya Kiranja wa Wengi katika Seneti, Dkt Irungu Kang’ata kumwandikia barua Rais akimwonya kwamba wananchi wengi eneo la Kati hawataki marekebisho ya katiba yalivyopendekezwa.

Kabla ya barua hiyo kuibua mdahalo mkali kuhusu hatima ya BBI, duru zilisema kitengo cha ujasusi kitaifa (NIS), tayari kilibainisha wapigakura wengi nchini hawataki kusakata densi ya Rais na Bw Odinga iliyo maarufu kama Reggae.

Wadau wengine wengi wakiwemo baadhi ya viongozi wa kidini na mashirika ya kijamii pia wamekuwa wakionya kuwa huu si wakati mwafaka wa kuendeleza mchakato wa kurekebisha katiba kwani taifa linakumbwa na changamoto tele hasa za kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tifa, ni asilimia 29 pekee ya Wakenya ambao wangepitisha marekebisho ya katiba endapo kura ya maamuzi ingefanyika wakati huu.

Kwa upande mwingine, asilimia 32 walisema wangepiga kura ya ‘la’ huku wale ambao wangesusia kura hiyo wakiwa asilimia 26, na wasiokuwa na uhakika kuhusu uamuzi wao wakiwa ni asilimia 16.

Hii ni kumaanisha kuwa, hata ikiwa wale ambao hawajafanya uamuzi kuhusu msimamo wao wakiamua baadaye kuunga mkono BBI, watafanya idadi ya wanaounga mkono ifike asilimia 45 pekee.

Vile vile, ni asilimia 44 pekee wanaokubaliana na pendekezo la kuandaa kura ya maamuzi kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022. Asilimia 12 wanataka kura hiyo ifanywe sambamba na Uchaguzi Mkuu, huku asilimia 31 wakitaka ifanywe baadaye.

Sababu kuu zilizotajwa za kupinga kura ya maamuzi ni kwamba hakuna maelezo ya kutosha kuhusu mapendekezo ya kurekebisha katiba (asilimia 32), kura ya maamuzi si muhimu wakati huu kwa sababu ya changamoto zinazokumba nchi (asilimia 20), mchakato mzima umeongeza taharuki ya kisiasa na migawanyiko (asilimia tisa) na mapendekezo ya kuongeza Rais mamlaka ni tishio kwa demokrasia (asilimia sita).

Wale ambao wameamua watasusia uchaguzi huo walisema hakuna maelezo ya kutosha kuhusu BBI (asilimia 68), na asilimia kumi wanaamini kutakuwa na ulaghai wakati wa kura ya maamuzi ili kuhakikisha mapendekezo hayo yamepitishwa kwa njia yoyote ile.

“Kwa jumla, kuna watu wachache mno ambao wanafahamu kuhusu mapendekezo ya BBI kwani asilimia 84 hawajui yaliyomo katika mswada wa mapendekezo ya kurekebisha katiba. Hii ni ishara kwamba inahitajika kuwe na hamasisho kwa umma ili Wakenya wafanye maamuzi wakiwa na ufahamu,” inaeleza ripoti hiyo.

Wale wachache ambao walisema wataunga mkono marekebisho ya katiba walisema wamevutiwa na mapendekezo ya kuongezwa fedha kwa kaunti (asilimia 19), nafasi za waziri mkuu na manaibu zitaleta uwakilishi wa jamii nyingi serikalini (asilimia 15), manufaa kwa vijana (asilimia tano) na atakayeibuka wa pili katika kura ya urais kuwa kiongozi wa upinzani bungeni (asilimia tano).

Cha kushangaza ni kuwa, asilimia 40 ya Wakenya waliosema wataunga mkono BBI hawana sababu zozote kuhusu uamuzi wao.

Hii ni ishara ya kuwa huenda wanafuata matakwa ya viongozi wa kisiasa bila kufahamu watakachopigia kura.

Ilibainika kuwa, wafuasi wa ODM ndio wengi zaidi miongoni mwa wanaounga mkono BBI (asilimia 66).

Ni asilimia 36 pekee ya wafuasi wa Rais Kenyatta ambao walisema wataunga mkono marekebisho ya katiba, huku kukiwa na asilimia 13 pekee ya wafuasi wa Naibu Rais, Dkt William Ruto ambaye hupinga BBI.

Matokeo haya yanawiana na onyo lililotolewa na Dkt Kang’ata kwa Rais, kwamba ngome yake itaangusha BBI.

Kuhusu mbinu ya kupigia kura marekebisho ya katiba, ni wachache (asilimia 37) ambao wanaunga mkono wito wa Bw Odinga kwamba kuwe na swali moja pekee la kupigiwa kura ya ndio au la.

Kulingana na utafiti, asilimia 46 wanaunga mkono pendekezo la Dkt Ruto na wandani wake kwamba endapo ni lazima kura ya maamuzi ifanywe, kila suala lililotajwa katika mswada liwe na swali lake ili wananchi waamue yale wanayotaka, na wakatae kile wanachoona hakifai.

Ripoti hiyo ilitolewa huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikiendelea kuthibitisha kama kuna sahihi milioni moja halali za wapigakura miongoni mwa zile zilizowasilishwa na waratibu wa BBI.

Habari zinazohusiana na hii

Acha katambe

Kwa nini tunapinga BBI

Hisia mseto kuhusu BBI