Wamukota asaini kandarasi kuendelea kuwa mchezaji wa Patriots Rwanda miaka miwili ijayo

Na GEOFFREY ANENE

MCHEZAJI wa kimataifa wa mpira wa vikapu Mkenya Bush Wamukota ataendelea kuwa mali ya mabingwa Rwanda, Patriots kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Hii ni baada ya mchezaji huyo wa kati, ambaye ni mwanawe mbunge wa Webuye West Daniel Wanyama Sitati, kuongezwa kandarasi hapo Januari 8, huku msimu 2020-2021 ukinukia.

Wamukota pamoja na mchezaji bora wa ligi hiyo msimu 2018-2019 Dieudonne Ndizeye, mshambuliaji Steven Hagumintwari na mlinzi Guibert Nijimbere walisaini kandarasi ya misimu miwili.

Patriots inanolewa na Mwamerika Dean Murray anayesaidiwa na Mkenya Bernard Oluoch na raia wa Burundi, Olivier Ndayiragije.

Wamukota alikosa mechi za Kenya Morans za raundi ya kwanza za Kundi B za kuingia Kombe la Afrika (AfroBasket) dhidi ya Senegal, Angola na Msumbiji mwezi Novemba 2020 akiwa karantini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Anatarajiwa kuwepo kwa raundi ya lala-salama timu hizo zitakaporudiana mwezi ujao hapo Februari 19-21.

Kaimu Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) Ambrose Kisoi alisema Januari 7 kuwa Morans itaanza matayarisho yake kabla ya Januari 15.

Kuna ripoti kuwa vijana hao wa kocha Cliff Owuor wataanza kujinoa Januari 9. Timu tatu bora kutoka orodha ya Kenya, Angola, Senegal na Msumbiji zitafuzu kushiriki AfroBasket baadaye 2021 nchini Rwanda.