Liverpool wazamisha makinda wa Aston Villa na kusonga mbele katika Kombe la FA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walifuzu kwa raundi ya nne ya Kombe la FA msimu huu wa 2020-21 mnamo Januari 8 baada ya kuwapepeta Aston Villa 4-1 ugani Villa Park.

Hata hivyo, masogora wa kocha Jurgen Klopp walihitaji mabao matatu ya kipindi cha pili ili kuzamisha chombo cha Villa waliotegemea idadi kubwa ya chipukizi katika akademia yao.

Mkurupuko wa virusi vya corona ulioshuhudiwa katika uwanja wa mazoezi wa Villa ulimaanisha kwamba hakuna mchezaji yeyote wa kikosi cha kwanza angenogesha kivumbi hicho.

Hivyo, Villa waliwajibisha wanasoka saba wa kikosi cha U-23 na wanne wengine katika kikosi chao cha U-18.

Licha ya kufungwa bao la mapema lililojazwa kimiani na Sadio Mane katika dakika ya nne, makinda wa Villa walisalia thabiti katika safu ya ulinzi huku Louie Barry, 17, akiduwaza wengi alipocheka na nyavu za Liverpool na kusawazisha mambo katika dakika ya 41.

Chipukizi huyo anayechezea kikosi cha U-17 katika timu ya taifa ya Uingereza, alizaliwa hatua chache kutoka ugani Villa Park na aliingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho mnamo Januari 2019 baada ya kusajiliwa kwa kima cha Sh112 milioni kutoka akademia ya Barcelona.

Hata hivyo, pumzi za matineja wengi wa Villa zilikwisha katika dakika ya 60 na hilo likawapa Liverpool fursa ya kupachika wavuni jumla ya mabao matatu chini ya kipindi cha dakika tano.

Georginio Wijnaldum alifunga goli la pili la Liverpool katika dakika ya 60 kabla ya Mane na Mohamed Salah kufunga mengine.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Villa, Christian Purslow, iliwawia vigumu kujaza idadi ya wanasoka wa kikosi cha kwanza na wale wa akiba kwa minajili ya mechi hiyo dhidi ya Liverpool kiasi kwamba baadhi ya wachezaji wao waliletwa uwanjani na wazazi wao ili kufanyiwa virusi vya corona.

Kati ya wanasoka waliounga kikosi cha kwanza cha Villa, wanne walikuwa na umri wa miaka 17 huku kiungo Benjamin Chrisene akiwa mchezaji mchanga zaidi (miaka 16) kuwajibishwa na Villa katika mechi hiyo.