• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Partey kurejea ugani kusaidia Arsenal kuanza kutetea ubingwa wa Kombe la FA dhidi ya Newcastle United

Partey kurejea ugani kusaidia Arsenal kuanza kutetea ubingwa wa Kombe la FA dhidi ya Newcastle United

Na MASHIRIKA

ARSENAL wataanza kutetea ufalme wa Kombe la FA kwa kualika Newcastle United ugani Emirates leo Jumamosi.

Kocha Mikel Arteta amefichua mpango wa kumpanga kiungo Thomas Partey katika kikosi cha kwanza atakachokitegemea kwenye mchuano huo.

Partey aliingia katika sajili rasmi ya Arsenal mwanzoni mwa msimu huu kwa kima cha Sh6.3 bilioni kutoka Atletico Madrid ya Uhispania.

Kwa upande wake, kocha Steve Bruce wa Newcastle amesema atakifanyia kikosi chake mabadiliko machache zaidi ikizingatiwa kwamba idadi kubwa ya wanasoka wake wanaugua Covid-19.

Martin Dubravka anatarajiwa kupangwa katikati ya michuma huku Ryan Fraser na Jamal Lewis wakisalia mkekani kwa sababu ya majeraha.

Hata hivyo, kikosi hicho kimepigwa jeki na marejeo ya nahodha Jamaal Lascelles ambaye amepona Covid-19. Nyota huyo anatarajiwa kushirikiana vilivyo na Alain Saint-Maximin ambaye pia amerejelea mazoezi baada ya kupona corona.

Arsenal wataingia ugani wakipania kuanza utetezi wao kwa matao ya juu ikizingatiwa kwamba wanajivunia motisha kubwa iliyowashuhudia wakiwapepeta West Bromwich Albion, Brighton na Chelsea katika michuano mitatu iliyopita katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kubwa zaidi linalotarajiwa kuchangia ari na motisha ya Arsenal ni rekodi nzuri wanayojivunia dhidi ya Newcastle. Arsenal wameshinda Newcastle 3-0 katika mechi zote tatu zilizopita za Kombe la FA. Mechi hizo ni za raundi ya tano mnamo 1936, robo-fainali mnamo 2002 na raundi ya nne mnamo 2008.

Arsenal wamedenguliwa kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA mara moja pekee katika kipindi cha misimu 24 iliyopita, na hiyo ilikuwa dhidi ya Nottingham Forest mnamo 2017-18.

Kwa upande wao, Newcastle wamebanduliwa mara 10 kwenye Kombe la FA katika kipindi cha misimu 11 iliyopita ambapo wamekutanishwa na washindani wenzao kwenye EPL. Mara ya pekee ambapo walifaulu kusonga mbele ni mnamo Januari 2012 walipopiga Blackburn Rovers 2-1 katika raundi ya tatu.

Katika kampeni za msimu uliopita WA 2019-20, Partey, 27, aliwajibishwa na Atletico katika mechi 35 za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na akafunga mabao matatu.

Mchango wake ulisaidia Atletico ya kocha Diego Simeone kukamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya tatu mnamo 2019-20. Hadi alipoaagana rasmi na Atletico, Partey alikuwa amechezea kikosi hicho mara 188 tangu ajiunge nacho mnamo 2011.

Kusajiliwa kwake na Arsenal kulifaulishwa na hatua ya kiungo raia wa Uruguay, Lucas Torreira, 24, kukamilisha uhamisho wake hadi Atletico kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Arsenal walianza kuyahemea maarifa ya Partey, ambaye amechezeshwa na Ghana mara 29, tangu mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2019-20.

Akiwa Atletico, kiungo huyo mkabaji alisaidia waajiri wake kutia kapuni ubingwa wa Europa League mnamo 2017-18 na taji la Super Cup mnamo 2018. Mafanikio yake katika soka ya La Liga yalichochea Atletico kumpa mkataba mpya wa miaka mitano mnamo 2018 na alitarajiwa kuendelea kuhudumu ugani Wanda Metropolitano hadi Juni 2023.

Kuja kwa Partey ugani Emirates kulichochea pia na hatua ya Arsenal kumwachilia kiungo Matteo Guendouzi, 21, kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Hertha Berlin kwa mkopo wa mwaka mmoja.

You can share this post!

Liverpool wazamisha makinda wa Aston Villa na kusonga mbele...

Mary Wambui apata kazi nyingine serikalini