• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wakenya kujaribu bahati yao kwa mara nyingine katika Mbio za Great Ethiopian Run

Wakenya kujaribu bahati yao kwa mara nyingine katika Mbio za Great Ethiopian Run

Na CHRIS ADUNGO

WAKENYA Solomon Boit, Evens Kipkemei na Kennedy Kimutai watakuwa miongoni mwa wanariadha 300 watakaonogesha mbio za kilomita 10 za Great Ethiopian Run mnamo Januari 10, 2021 jijini Addis Ababa.

Mshindi wa makala ya 20 ya mbio hizo zitakazoandaliwa katika uwanja wa Meskel Square atatia mfukoni kima cha Sh280,000.

Baadhi ya Waethiopia watakaotoana kijasho na Wakenya kwenye mbio hizo ni bingwa mara mbili wa mita 5,000 duniani Mukhtar Edris na Abe Gashahun aliyetawazwa mfalme wa Riadha za Great Ethiopian Run mnamo 2016.

Ethiopian Run ni miongoni mwa mbio maarufu ambazo zimekuwa zikivutia ushiriki wa kiwango cha juu katika ulingo wa riadha barani Afrika.

Kivumbi hicho kiliasisiwa na nguli wa riadha nchini Ethiopia, Haile Gebrselassie ambaye ni mshikilizi wa zamani wa rekodi za dunia katika mbio za marathon na mita 10,000.

Kwa miaka kadhaa iliyopita, Gebrselassie amekuwa akiwekeza fedha zinazotokana na ushiriki wa mbio hizo kuwekeza kwenye miradi ya kuwafaidi wanajamii nchini Ethiopia, mradi wa hivi karibuni ukiwa ni ujenzi wa shule kwa ushirikiano na Serikali Kuu ya Jamhuri ya Ethiopia.

Miongoni mwa wageni mashuhuri walioalikwa kuhudhuria hafla ya ufunguzi wa mbio hizo mwaka huu ni Mkenya Paul Tergat aliyekuwa mshindani mkuu wa Gabreselassie katika enzi zao za utimkaji.

Ingwa hivyo, Tergat hakuhudhuria hafla ya ufunguzi wa mbio hizo mnamo Januari 8, 2021 kwa kuwa anashughulikia kaka na baadhi ya jamaa zake waliohusika kwenye ajali ya barabarani hivi majuzi katika Kaunti ya Baringo.

“Bila Tergat, mchezo wa riadha usingekuwa wa kuvutia zaidi kwangu jinsi ilivyoishia kuwa. Ni miongoni mwa marafiki zangu wakuu na ingawa hayuko katika hafla hii, nahisi kana kwamba yuko tu,” akasema Gebreselassie katika hafla hiyo ya Ijumaa iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Utamaduni na Utalii nchini Ethiopia, Habtamu Sisay Awas.

Wengine waliohudhuria ni bingwa wa zamani wa dunia katika Mbio za Nyika, Gebregziabher Gebremariam na Million Wolde aliyeibuka mshindi wa mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za mwaka 2000 jijini Sydney, Australia.

“Mbio za Great Ethiopian Run zimekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza utajiri wa vipaji vinavyojivuniwa na Waethiopia katika ulingo wa riadha. Ni mashindano ambayo pia yamewezesha taifa la Ethiopia kukuza sekta ya utalii na kudumisha amani, upendo, umoja na utangamano wa kijamii,” akasema Waziri Awas.

Kwa mujibu wa Ermias Ayele ambaye ni meneja wa mbio hizo, makala ya mwaka huu yalitarajiwa kunogeshwa na zaidi ya wanariadha 50,000 ila idadi hiyo ikapunguzwa katika jitihada za kuzingatia baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mawazo asili ya kuanzishwa kwa mbio hizo yalitolewa na bingwa wa zamani wa Hamburg Marathon, Richard Nerurkar ambaye ni raia wa Uingereza, Gebrselassie na Ayele.

Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita tangu mashindano hayo yaanzishwe, hakuna mwanariadha asiye Mwethiopia ambaye amewahi kuibuka mshindi wa kwanza.

Wanariadha wote 300 watakaoshiriki makala ya mwaka huu yalifanyiwa vipimo vya Covid-19 mnamo Januari 8 katika ukumbi wa Millenium Hall jijini Addis Ababa.

Mbio za Ethiopian Great Run zimekuwa zikiandaliwa kila mwaka katika mwezi wa Novemba. Hata hivyo, mashindano ya mwaka uliopita wa 2020 yaliahirishwa kwa sababu ya corona.

  • Tags

You can share this post!

Oliech kuandaa mechi kubwa ya kuwapa mashabiki fursa ya...

Wakenya wengi hawataki BBI – Utafiti