RIZIKI: Ushonaji nguo unahitaji utafiti wa kutosha kuelewa soko

Na SAMMY WAWERU

SEKTA ya mitindo na muundo wa mavazi hapa nchini na pia kiwango cha kimataifa ni yenye ushindani mkubwa kutokana na kuendelea kuimarika kwa teknolojia.

Ni sekta inayohitaji wanafasheni na mafundi kuwa ngangari, na kuenda na nyakati.

Muundo wa nguo ulio maarufu leo, sio utakaokuwa maarufu baada ya mwaka mmoja, kipindi kama hiki.

Muundo na fashioni nyingine itakuwa imeibuka, jambo ambalo linaleta ushindani wa aina yake miongoni mwa mafundi ili kuafikia matakwa na mapenzi ya wateja.

Kijana Amani Ruhimbana amekuwa fundi wa nguo kwa muda wa miaka 12 mfululizo. Kipindi hicho kimemuwezesha kuwa fundi mwanamitindo stadi.

Ni kipindi ambacho kimempa tajiriba, akawa fundi anayetambua ndani na nje ya sekta ya mitindo na muundo wa nguo.

Anafahamu bayana ushindani uliopo katika soko la uanamitindo wa mavazi, na ili kuuwahi yeye na utafiti ni kama chanda na pete.

Makala ya fashioni mpya ya nguo yanayochapishwa kwenye magazeti na majarida, hakosi kuyachambua kwa minajili ya kujua mapya.

“Vipindi vya mitindo kwenye runinga vinapopeperushwa huhakikisha havinipiti,” Ruhimbana anadokeza.

Yote tisa, kumi ni mtafiti wa kina katika mitandao ya kijamii, hususan kwenye kurasa na makundi ya mitindo na muundo wa mavazi, shabaha ikiwa kujua ni fashioni ipi imeibuka.

“Kuendelea kuimarika kwa teknolojia kumerahisisha kazi, fashioni mpya inapojiri intaneti ndio ukumbi wa kwanza kuchapishwa,” anaelezea.

Ni jitihada ambazo zimemuwezesha Ruhimbana, 31, kuwa fundi wa kipekee, na kuenda na wakati.

Duka lake la ushonaji nguo lililoko eneo la Progressive, mtaani Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi, amewekeza katika kila aina ya fasheni.

Amani Ruhimbana ni fundi wa mavazi ya mitindo ya Kiafrika. Picha/ Sammy Waweru

La mno ni fundi wa mavazi yenye asili ya Kiafrika, maarufu kama Ankara. Hutumia vitambaa vya kitenge kushona mavazi hayo.

“Sababu hasa ya kuamua kukumbatia Ankara ni kudumisha mila na tamaduni zetu za Kiafrika,” anasisitiza Ruhimbana ambaye ni mkimbizi hapa nchini Kenya.

Kijana huyu ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alitua Kenya mwaka wa 2007 kutafuta amani, baada ya vita vya ndani kwa ndani kuzuka nchini humo.

Kishonge anasifia utulivu na amani inayosheheni Kenya, akisema imemfanya kuwa kati ya wanaotegemewa katika sekta ya mitindo na muundo wa nguo.

Anafichua kwamba alipowasili nchini kama mkimbizi, alichukuliwa na Umoja wa Mataifa (UN)n na kupelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyoko Kaunti ya Turkana.

Alifanya vibarua vya kupigia watu nguo pasi, katika maduka ya mafundi aliounda urafiki nao. Katika harakati za kufanya shughuli hizo kupata angaa hela kukidhi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi, alijifunza kukarabati na kushona nguo.

“Mwaka wa 2008 UN ilitoa ufadhili kwa vijana kadha kambini kusomea kozi mbalimbali za kiufundi. Nilikuwa miongoni mwa waliobahatika, nikachagua uanamitindo na muundo wa nguo,” anafafanua.

Aidha, barobaro huyu alikuwa kati ya wanafunzi bora, msingi wa ushonaji uliomuwezesha kuwa fundi hodari.

Mavazi yenye asili za Kiafrika, hushona suti za kike na kiume, zinazoandamana na viatu vya vitenge vigumu.

“Suti huandamanisha na viatu ninavyounda,” asema.

Hali kadhalika, hushona suruali ndefu, kaptura, blauzi, sketi, magauni, kofia, jaketi, mikoba ya wanawake na pia ya wanaume, kwa kutumia vitenge.

Viatu anavyotengeneza vinajumuisha vya spoti, loafers, kati ya vinginevyo kulingana na maelezo ya mteja.

“Ukitaka mashuka ya kitanda, duvets, kava zozote zile zikiwemo za magari nitakushonea,” anadokeza fundi huyu.

Ni ustadi wa kipekee uliomuwezesha kutangamana na baadhi ya wasanii na wanamuziki nchini.

Huku lengo lake likiwa kudumisha mila na tamaduni za Kiafrika, Amani Ruhimbana pia hushona mavazi ya mitindo na miundo ya kisasa, inayotumia vitambaa vya kawaida.

Bei za bidhaa zake ni kati ya Sh300 hadi Sh3,500.

“Changomoto hazikosi. Kipindi hiki cha janga la Covid-19 sawa na biashara zingine, sekta ya mitindo na muundo wa mavazi hasa kwetu mafundi tumeathirika. Mauzo yamekuwa yamedidimia nikilinganisha na miaka ya awali,” anaelezea, akiwa mwingi wa matumaini mwaka mwaka huu wa 2021 mambo yatakuwa shwari.

Virusi hatari vya corona na ambavyo vimehangaisha uchumi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni vilitua nchini mnamo Machi 2020.

Kupata duka liloloko sehemu bora kuvumisha huduma zake pia Ruhimbana anasema imekuwa kibarua.

Licha ya hayo, anasema muhimu zaidi ni mchango anaoleta katika sekta ya nguo.

“Utafiti wa kina ndio nguzo ya ufanisi katika sekta ya uanamitindo na muundo wa mavazi,” anasisitiza, kauli yake ikipigwa jeki na Elizabeth Wakaguyu ambaye ni fundi wa nguo za kike jijini Nairobi.

“Fashioni ya nguo inaenda na wakati, ni muhimu kuwa mtafiti na kujua ni muundo upi unavuma sokoni,” Elizabeth anaelezea.

Ruhimbana hutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp kuvumisha huduma zake. Ni mchipuko wa teknolojia ya kisasa anaosema umemsaidia kwa kiasi kikubwa kupata wateja.