• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Chama cha Pwani ni Kadu Asili – Jumwa

Chama cha Pwani ni Kadu Asili – Jumwa

Na MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Malindi Bi Aisha Jumwa, amefichua kuwa Chama cha Kadu Asili kinapigwa msasa ili kiwe chama rasmi cha Wapwani. Bi Jumwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, wamekuwa mstari wa mbele kupigania hitaji la eneo hilo kuwa na chama ambacho jamii inaweza kujitambulisha nacho, sawa na ilivyo katika kanda nyingine za nchi.

Hata hivyo, mpango huo hupata pingamizi kutoka kwa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho ambaye anaamini masuala ya Wapwani hutetewa vyema kupitia Chama cha ODM.Bw Joho husema kuwa wanaojitokeza kutaka chama cha Wapwani wana nia za kibinafsi kwani wanataka kupeleka kura za eneo hilo kwa mtu binafsi.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Jumapili jana, Bi Jumwa alisema anaunga mkono Kadu Asili na kutaka viongozi waliotaka chama wa Wapwani wajiandae kuingia katika chama hicho.

Mbunge huyo alisema kuwa wakati Gavana Joho na wabunge wengine wa ODM waliamua kukosoa chama hicho kuendelea kukitumia, wao walikuwa wanajikuna kichwa kuhusu jinsi gani Pwani itakuwa na sauti katika siasa za kitaifa za mwaka wa 2022.

“Wakati walikuwa wameganda kama gamu sisi tulikuwa tunafanya kupekua ni hatua gani mwafaka itakayotufaa na sasa tumemaliza, chama kipo tayari,” akasema. Alimtaka Bw Joho kujikaza kibwebwe na kuwa tayari kukabiliana na chama hicho cha Pwani uwanjani.

Bi Jumwa ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alidai kuwa waasi wa ODM katika eneo la Pwani wametimiza maombi na azimio la Gavana wa Kilifi Amason Kingi la kuwepo kwa chama cha Pwani kitakachopigania matakwa ya eneo hilo katika uchaguzi mkuu wa 2022. “Kingi alisema nasi tumetimiza,” akasema Bi Jumwa.

Akizungumza katika sherehe ya kumkaribisha kasisi Alphonce Mwaro wa kanisa ya ACK Mombasa mwaka wa 2018 mwezi mmoja kabla ya handisheki, Gavana Kingi alisema Pwani haitaunga mkono chama chochote cha siasa ambacho si cha Pwani ifikapo 2022. Kulingana Jumwa chama cha ODM kiliwasaliti Wapwani.

“Tulifanyia ODM kampeni nchi mzima na kukiunga mkono mia kwa mia kama wa Pwani kwa sababu manifesto yake ilikuwa sawa na changamoto zinakokumba eneo la Pwani,” akasema Bi Jumwa.

Alisema kuwa wanasiasa wanafaa kuiga mwanzilishi wa chama cha KADU marehemu Ronald Gideon Ngala ambaye alijilotea kupigania haki ya Wapwani kupitia chama chake bila ubinafsi. Wakati huo huo, alisisitiza kuwa Bw Joho hawezi kuwakilisha Wapwani katika nyanda ya kisisasa akiwa katika chama cha ODM.

“Joho atakuwaje mgongo wa Wapwani chini ya makwapa ya mtu mwingine?” akauliza Bi Jumwa.Alikejeli hatua ya Bw Joho kutawazwa kama kigogo wa eneo la Pwani na wazee kutoka Kaunti ya Tana River wiki iliyopita

You can share this post!

Yattani apondwa kuhusu ongezeko la deni la kitaifa

Kioni asutwa kwa madai hakumpigia kura Mudavadi alipokuwa...