Kioni asutwa kwa madai hakumpigia kura Mudavadi alipokuwa mgombea mwenza

DERRIC LUVEGA na VALENTINE OBARA

ALIYEKUWA Mbunge wa Ndaragua, Bw Jeremiah Kioni, Jumamosi alipigiwa kelele katika mazishi ya mamaye Kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi.

Waombolezaji walionekana kukumbuka kuhusu habari zilizoenezwa kwamba Bw Kioni hakumpigia kura Bw Mudavadi wakati alipokuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais mwaka wa 2013.Hata hivyo, Bw Kioni alijikakamua na kueleza waombolezaji kuwa habari hizo zilikuwa za uongo.

“Ukweli ni kwamba hayo yote yalikuwa uongo. Nilimpigia kura Mudavadi,” akasema.Alieleza kuwa, wakati Bw Mudavadi alipopokea habari hizo, alimtafuta wakazungumza. Alimsifu kiongozi huyo wa ANC kwa kumpa muda kujieleza.“Kama mwanasiasa, angenifukuza na kunitusi lakini yeye na mkewe waliniuliza kilichokuwa kikiendelea,” akasema.

Bw Mudavadi, ambaye aliondoka kitini mwake na kusimama kando ya Bw Kioni ili kutuliza hasira za umati, aliwakemea waliosambaza habari hizo sawa na walioziamini.

“Wengi wenu mliamini uongo huo, aibu kwenu. Inafaa tukome kuamini uongo hii Kenya. Jeremiah amesimama hapa kwa ujasiri kwa sababu anajua ukweli uliotendeka wakati huo.” akasema.

Bw Mudavadi aliwakashifu waombolezaji waliomzomea Bw Kioni kwa kugeuza matanga kuwa eneo la makabiliano ya kisiasa.

“Tulikuja kwa mazishi ya mama Hannah wala si ushindani wa kisiasa,’ akasema Bw Mudavadi.Alimtetea Bw Kioni na kusema kwamba alitengwa na wengi kisiasa katika eneobunge lake kwa kusimama naye badala ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye ndiye alikuwa na ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya.