• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Uhuru anguruma, aashiria atamruka Ruto urais 2022

Uhuru anguruma, aashiria atamruka Ruto urais 2022

DERRIC LUVEGA na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa ishara kubwa kwamba huenda hatamuunga mkono naibu wake, Dkt William Ruto kwa urais ifikapo mwaka wa 2022.

Akijibu wito wa viongozi waliomtaka ‘awachape’ viboko wanasiasa wa Chama cha Jubilee wanaoegemea upande wa Dkt Ruto, Rais alisema wanaogawanya nchi kwa matabaka ya matajiri na maskini wanafaa wajihadhari.

Kwa muda mrefu sasa, Dkt Ruto na wandani wake katika kikundi cha Tangatanga wamekuwa wakiendeleza siasa za kuashiria nchi imetekwa na matajiri, wakidai Dkt Ruto ni mtetezi wa maskini almaarufu ‘hasla’.

Hata hivyo, akizungumza jana wakati wa mazishi ya Hannah Mudavadi ambaye ni mamaye kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi katika Kaunti ya Vihiga, Rais Kenyatta alisema wanaodai wamechoshwa na jinsi familia chache zinavyoongoza nchi wanafaa pia wazingatie ni jamii mbili pekee ambazo zimewahi kutawala nchi hii.

Tangu Kenya ilipopata uhuru, marais wamekuwa wa jamii za Wakikuyu na Wakalenjin, huku Dkt Ruto pia akiwa ni wa jamii ya Wakalenjin.

“Wacha pia mimi niseme. Kuna jamii mbili ambazo zimetawala, labda sasa ni nafasi ya jamii nyingine kutawala… au namna gani? Jamii za Kenya ni nyingi. Usiwe tu wa kutupatupa maneno. Tunataka Kenya thabiti ya watu milioni 48,” akasema.

Alisisitiza kuwa nia yake ni kuondoka mamlakani 2022 taifa likiwa lenye umoja. Kabla ahutubu, viongozi wengi waliomtangulia walitoa changamoto kwake achukue hatua dhidi ya viongozi wa Tangatanga, ambao kulingana nao wamemkosea Rais heshima.

“Baba yako (Mzee Jomo Kenyatta) alikuwa anaita hao watu vinyangarika. Chukua hatua. Usipochunga utawakuta chumbani mwako na wewe ndiwe utapata hasara. Tunakusaidia ilhali hutoki nje kutusaidia kulisha watu viboko? Linda wanajeshi wako. Toka nje! Toka nje!” alisema Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli.

Rais alipohutubu, alijibu kwa kusema: “Msione simba amenyeshewa mkafikiria ni paka. Kila kitu na wakati wake. Watu wafanye kile wanachotaka lakini mjue mimi ndiye rais wa nchi hii, na najua kile ninachofanya.”

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka miongoni mwa wengine.

You can share this post!

Kioni asutwa kwa madai hakumpigia kura Mudavadi alipokuwa...

Mwana anaswa kwa mauaji ya watu 5 wa familia yake