• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mwanaume akata mkewe miguu kwa kumtoroka

Mwanaume akata mkewe miguu kwa kumtoroka

Na WYCLIFFE NYABERI

MWANAMKE katika Kaunti ya Kisii anauguza majeraha mabaya ya upanga hospitalini baada ya mumewe kumkata miguu akidai mke huyo alimwacha nyumbani kisha akaenda kuolewa kwingine.

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Bomware, eneobunge la Mugirango Kusini.Kulingana na naibu chifu Robert Juma wa eneo husika, Bi Naomi Bosibori, 22, aliondoka nyumbani kwa mumewe James Oroko wiki tatu zilizopita kumtembelea shangaziye katika eneo la Etago.

Baada ya kukaa na shangazi kwa wiki moja, ilisemekana mwanamke huyo alienda kuishi na mwanamume mwingine hapo kijijini waliyejuana kwa kipindi hicho kifupi.

Haukupita muda mrefu kabla uvumi kuenea kwamba Bi Bosibori alikuwa amemwacha mumewe na kuolewa kwingine, kisha mumewe akapokea habari hizo.

Akiwa amebeba upanga mkali mnamo Ijumaa alasiri, mwanaume huyo alifunga safari hadi kwa boma ambapo Bi Naomi alikuwa ametorokea, na kumfuata chumbani kisha akaanza kumkatakata mwili mzima.

Alimdhuru sana miguuni kwa upanga kiasi cha kwamba miguu yake ilibaki imeshikiliwa na ngozi pekee. Mwathiriwa alikatwa vibaya pia mikononi.“Alipoona anamalizwa, alipiga ukemi mkali uliowavutia wanakijiji waliofika kumwokoa.”

Kwa huzuni waliyoona, raia walimgeukia mwanaume huyo na kuanza kumpiga kwa mawe na upanga waliompokonya. Kwa bahati nzuri nilifika mapema na kumwokoa jamaa huyo kutokana na hasira za wenyeji japo pia alipata majeraha kiasi,” akasema chifu.

Kwa ushirikiano wa chifu na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Nyamaiya, wawili hao walikimbizwa hospitali ya kimisheni ya Tabaka kupata matibabu.Taifa Jumapili ilipofika hospitalini humo jana mchana, mwathiriwa alikuwa amehamishiwa hospitali nyingine kupokea matibabu maalumu.

“Hatungeweza kuyamudu majeraha yake kwa hivyo tuliwaelekeza waliokuja naye wakampeleke kwingine haraka iwezekanavyo,” akasema muuguzi aliyeomba jina lake libanwe kwa kuwa hana ruhusa ya kuongea na wanahabari.Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Kisii, Bw Jebel Munene alisema kwa njia ya simu kuwa mwanaume huyo alikamatwa na atafunguliwa mashtaka pindi tu atakapoondoka hospitalini.

Polisi walihifadhi upanga uliotumika katika uovu huo na silaha nyingine zitakazotumika kama ushahidi dhidi yake atakapofikishwa mahakamani.

You can share this post!

Malala amtaka Rais kuadhibu wanaomsumbua chamani

MTG United yaiadhibu Limuru Starlets 4-0