Matiang’i kupewa fimbo ya kuongoza jamii ya Gusii kisiasa

Ruth Mbula na Benson Ayienda

WAZIRI wa Usalama Dkt Fred Matiang’i anaelekea kuidhinishwa kuwa msemaji rasmi wa jamii ya Wagusii katika masuala ya siasa za kitaifa.

Viongozi wa kisiasa kutoka jamii hiyo jana waliambia wazee wa Baraza la Jamii ya Abagusii kwamba, wamemteua Dkt Matiang’i awe msemaji wa kijamii.Jamii hiyo imekosa msemaji kwa muda mrefu baada ya aliyekuwa waziri wa fedha, Bw Simeon Nyachae, kujiuzulu kisiasa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Dkt Matiang’i, ambaye alihudhuria mkutano wa faraghani na viongozi hao jana, alisema mipango hiyo ni mema lakini atatangaza uamuzi wake baada ya kushauriana na Rais Uhuru Kenyatta.

Hii huenda ikawa ni kwa sababu mawaziri hawaruhusiwi kujihusisha na siasa. “Tunataka kuwa na msemaji wa jamii, ndiposa tulikutana hapa leo kumfahamisha waziri kuhusu mipango yetu,” mwenyekiti wa baraza hilo la wazee, Bw James Matundura, alisema baada ya mkutano wa jana.

Awali, Dkt Matiang’i aliongoza wanataaluma mbalimbali kutoka eneo la Gusii kutoa mchango wa Sh6 milioni kusaidia kwenye ujenzi wa madarasa ya kisasa katika Shule ya Msingi ya Egetonto, eneo la Mugirango Kusini, Kaunti ya Kisii.Dkt Matiang’i, ambaye ndiye mwenyekiti Chama cha Wanataaluma wa Jamii ya Gusii (GPA), aliizuru shule hiyo akiandamana na Katibu wa Wizara ya Afya, Dkt Susan Mochache na wanachama wengine wa kundi hilo.

Mwenyekiti wa kundi ni mwenyekiti wa Idara ya Kitaifa ya Kusimamia Ujenzi (NIB), Bw Moses Nyakiogora.

Wanachama wengine ni mwenyekiti wa Bodi ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) Mohamed Nyaoga, Naibu Mwanasheria Mkuu Ken Ogeto na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Kenya Commercial (KCB), Bw Joshua Oigara.Karibu Sh 700,000 kati ya zile zilizokusanywa zilitumika kununua ekari moja ya shamba ambako madarasa hayo yatajengwa.

Mbunge wa eneo hilo Silvanus Osoro amefadhili ujenzi wa madarasa mawili huku serikali ya kaunti hiyo ikiahidi kufadhili ujenzi wa darasa moja.