• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Sonko agundua kumbe Nairobi ina wajanja kumliko

Sonko agundua kumbe Nairobi ina wajanja kumliko

Na COLLINS OMULO

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, aliingia kwenye mtego wa mahasimu wake kisiasa jijini bila kujua, duru zimefichua.

Wanasiasa waliokuwa mstari wa mbele kupanga mikakati ya kumtimua Bw Sonko, jana walifichulia Taifa Leo kwamba, Chama cha Jubilee hakikuwa na mipango yoyote ya kuandaliwa uchaguzi mdogo baada ya gavana huyo kuondolewa mamlakani.

Hivyo basi, hatua ya Bw Sonko kukimbia mahakamani kuzuia uchaguzi mdogo ilikuwa baraka kwa Jubilee.Mnamo Jumamosi, Bw Sonko, kama kwamba aligundua kuchelewa kuna wajanja wa jiji kumliko, alitangaza amepanga kuondoa kesi zote kuhusu ugavana wa Nairobi alizowasilisha kortini.

Chama hicho kilitaka naibu gavana mteule, Bi Anne Mwenda Kananu aingie mamlakani na kama hilo halingewezekana, aliyekuwa naibu gavana Polycarp Igathe angeshawishiwa kurudi kwa siasa kwani Jubilee haikuwa imekubali kujiuzulu kwake kama naibu gavana.

Duru ziliongeza kuwa, wakuu wa chama walizingatia pia kumsimamisha Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja kwa ugavana lakini wazo hilo likafutiliwa mbali kwa vile ingemaanisha kungekuwa na uchaguzi mdogo wa useneta.

“Uchaguzi mdogo ungehitaji mabilioni ya pesa na hilo lilikuwa linaepukwa,” akasema mdokezi wetu. Maafisa katika Chama cha ODM walisema, mipango hiyo ilifahamika vyema na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wao Raila Odinga.

ODM inatarajiwa kupewa nafasi ya naibu gavana mpya, baada ya gavana atakayechukua mahali pa Sonko kuapishwa.

“Mnafikiria ni kwa nini hatukutangaza wagombeaji wetu? Tulifahamu vyema hata kabla gavana atimuliwe kwamba nafasi ya naibu gavana itaenda kwa ODM,” akasema afisa aliyezungumza na Taifa Leo.

Mnamo Jumatatu wiki iliyopita, Mahakama Kuu ilifutilia mbali ilani ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyokuwa imepanga uchaguzi mdogo Nairobi.

Hii ni baada ya Bw Sonko kuwasilisha kesi mahakamani kupinga uchaguzi mdogo. Punde baada ya Bw Sonko kusherehekea ushindi wake kortini dhidi ya IEBC, Bw Peter Agoro ambaye alikuwa amepinga uteuzi wa Bi Mwenda kuwa naibu gavana, aliwasilisha notisi mahakamani kuondoa kesi yake. Ombi lake lilikubaliwa.

You can share this post!

Tangatanga wamzomea Uhuru kwa matamshi

Wiper kumtia adabu Muthama kupitia mke waliyeachana