Wenyeji watawala mbio za Great Ethiopian Run, Wakenya watupwa nje

Na ELIAS MAKORI (akiwa Addis Ababa)

WENYEJI Waethiopia waliendeleza ubabe wao katika mbio za kilomita 10 za Great Ethiopian Run zilizoandaliwa Jumapili ya Januari 10, 2020 jijini Addis Ababa.

Wakenya wote waliokuwa wakishiriki makala ya 20 ya mbio hizo mwaka huu wa 2021 walitupwa nje ya mduara wa 20-bora.

Abe Gashahun aliibuka mshindi wa mbio hizo baada ya dakika 28:19.10, sekunde moja chini ya rekodi ya miaka 15 iliyowekwa na Deriba Merga. Ufanisi huo ulimfanya Gashahun kuwa mwanariadha wa tatu baada ya Hagos Gebrhiwet (2012, 2018) na Azmeraw Bekele (2010, 2014) kutawazwa mfalme wa mbio hizo mara mbili.

Tsigie Gebrselama aliyejizolea nishani ya shaba katika Mbio za Nyika za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2019, aliibuka mshindi wa kitengo cha wanawake baada ya dakika 32:33. Gebrselama aliibuka pia mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 3,000 kwenye Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2018 jijini Tampere, Finland.

Kennedy Kimutai (29:50.16), Solomon Boit (30:15.16) na Evans Kipkemei (30:50.66) waliokuwa wawakilishi wa Kenya katika mbio hizo waliambulia nafasi za 21, 27 na 35 mtawalia baada ya kulemewa na hali ya hewa nchini Ethiopia.

Jiji la Addis Ababa liko katika eneo la mita 2,355 juu ya usawa wa bahari, urefu unaoelekea kuwiana na eneo la Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet (mita 2,400). Mji wa Eldoret unafuata kwa karibu (mita 2,090).

Hakuna mwanariadha yeyote asiye mzawa au raia wa Ethiopia ambaye amewahi kutamalaki mbio za Great Ethiopian Run tangu ziasisiwe mnamo 2001.

“Barabara ilikuwa na milima mingi na hali ya hewa ilikuwa mbaya. Mwili wangu ulikataa kabisa kusonga kwa kasi jinsi nilivyotarajia,” akasema Boit ambaye hushiriki mazoezi yake katika eneo la Iten chini ya uelekezi wa kocha veterani Colm O’Connell.

“Tulianza vyema na tukawa miongoni mwa wanariadha waliotawala kundi la kwanza hadi mwisho wa kilomita tano. Kufikia hatua hiyo, nilihisi kulemewa na mwili ukaanza kuwa dhaifu,” akaongeza Boit aliyeambulia nafasi ya nne kwenye mbio za mita 10,000 katika Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2018. Mkenya Rhonex Kipruto alitamalaki mbio hizo zilizoandaliwa jijini Tampere, Finland.

Boit alisema kwa sasa analenga kuelekeza mawazo yake kwenye mchujo wa mbio za mita 10,000 kwa matarajio kwamba atapata jukwaa la kushirikiana vilivyo na Kibiwott Kandie ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya Half Marathon kumzamisha Joshua Cheptegei wa Uganda kwenye Olimpiki zijazo za Tokyo, Japan.

“Nilikubaliana na kocha Colm kwamba mbio za Great Ethiopia Run zitakuwa zangu za mwisho barabarani. Sasa napania kurejea uwanjani kujifua vilivyo kwa Olimpiki,” akasema.

Kipkemei na Kimutai pia walilalamikia hali mbovu ya hewa huku wakisisitiza kwamba walijifurahia kasi waliyoanza nayo mbio hizo kabla ya kibarua kuwa kigumu baada ya hatua ya kilomita tano za mwanzo.

Mnamo 2016, Geshahun aliyeibuka mshindi kwa muda dakika 28:53 alimzidi ujanja Mkenya Jorum Lumbasi (28:54) katika hatua ya mwisho na kutia kapuni taji lake la kwanza katika mbio hizo zilizoasisiwa na nguli wa riadha nchini Ethiopia, Haile Gebrselassie ambaye ni mshikilizi wa zamani wa rekodi za dunia katika mbio za marathon na mita 10,000.

Nafasi ya pili iliyoshikiliwa na Lumbasi (2016) na Nathan Naibei (2005) ndiyo nambari bora zaidi ambayo Wakenya wamewahi kuweka katika mbio hizo. Nicholas Kipkemboi aliambulia nafasi ya tatu mnamo 2011.

Mnamo Januari 10, Gashahun ambaye hukimbilia kikosi cha Elite Sports Management, alitawala makala ya mbio hizo mwaka huu bila ya ushindani wowote baada ya kuwekewa kasi ya kutosha na Waethiopia wenzake Milesa Mengesha na Tadese Worku wa kikosi cha Demadona Athletics Promotion.

Kwa upande wa wanawake, Gebrselama wa kikosi cha Ethio Athletics alikosa mshindani wa kumtoa kijasho na akafika utepeni baada ya dakika 32:33, muda uliokuwa mbali na dakika 31:55 ambao ni rekodi ya kasi zaidi iliyowekwa na Yalemzerf Yehualaw mnamo 2019. Yehualaw aliibuka mshindi wa nishani ya shaba kwenye Riadha za Nusu Marathon ya Dunia jijini Gdynia, Poland miezi mitatu iliyopita.

Gebrselassie alianziasha makala ya mbio za Great Ethiopian Run mwaka huu na akaongozwa hafla ya kutuzwa kwa washindi akisaidiwa na Gete Wami, Aselefech Mergia na Berhane Adere ambao pia ni majagina wa mbio za masafa marefu nchini Ethiopia.

Awali, makala ya mwaka huu yalitarajiwa kunogeshwa na zaidi ya wanariadha 50,000 ila idadi hiyo ikapunguzwa hadi 12,500 katika jitihada za kuzingatia baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mbio za Ethiopian Great Run zimekuwa zikiandaliwa kila mwaka katika mwezi wa Novemba. Hata hivyo, mashindano ya mwaka uliopita yaliahirishwa kwa sababu ya corona.

“Mbio za Great Ethiopian Run zimekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza utajiri wa vipaji vya wanariadha wetu. Ni mashindano ambayo pia yamewezesha taifa la Ethiopia kukuza sekta ya utalii na kudumisha amani, upendo, umoja na utangamano wa kijamii kiasi kwamba kwa sasa ni sehemu ya maisha yetu,” akasema Gebrselassie.

Kwa miaka kadhaa iliyopita, Gebrselassie amekuwa akiwekeza fedha zinazotokana na ushiriki wa mbio hizo kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kuwafaidi wanajamii wasiojiweza kifedha nchini Ethiopia. Mradi wa hivi karibuni ambao amekuwa akiushughulikia ni wa ujenzi wa shule kwa ushirikiano na Serikali Kuu ya Jamhuri ya Ethiopia.

MATOKEO YA MBIO ZA GREAT ETHIOPIAN RUN:

Wanaume:

  1. Abe Gashahun (Elite Sports Management) 28:19
  2. Tadese Worku (Demadona Athletics Promotion) 28:20
  3. Milkesa Mengesha (Elite Sports Management) 28:39
  4. Dagnachew Adere (Commercial Bank Sports Club) 28:53
  5. Lencho Tesfaye (Gelan Athletics Sports Club) 29:00

Women

  1. Tsigie Gebreselama (Ethio Athletics) 32:33
  2. Medihen Gebreselasie (Commercial Bank Sports Club) 32:35
  3. Gebeyanesh Ayele (Defence/Mekelakeya) 32:45
  4. Bosena Mulate (Amhara Maremiya) 32:52
  5. Melkenat Wedu (Debre Berhan University) 32:55

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

Habari zinazohusiana na hii