• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Afueni kwa shule 6 kufunguliwa baada ya miaka saba

Afueni kwa shule 6 kufunguliwa baada ya miaka saba

NA KALUME KAZUNGU

AFUENI imepatikana kwa zaidi ya wanafunzi 400 wa shule sita zilizoko msitu wa Boni zilizofungwa kwa miaka saba, Kaunti ya Lamu baada ya serikali kupeleka walimu na kuzifungua shule hizo.

Katika kipindi cha juma moja tangu shule kufunguliwa kote nchini, wanafunzi wa shule za Bodhai, Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe walilazimika kusalia nyumbani baada ya walimu kukosa kufika shuleni kufuatia changamoto ya usalama barabarani inayochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Mwishoni mwa juma, serikali ilipeleka zaidi ya walimu kumi kwenye shule hizo na kuamuru shule zote kufunguliwa ili wanafunzi wa msitu wa Boni wasome kama wengine.

Walimu hao walisafirishwa shuleni kupitia usafiri wa angani.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema wameweka mikakati kabambe, ikiwemo kudhibiti vilivyo usalama kwenye vijiji vyote vya msitu wa Boni katika juhudi za kuhakikisha masomo yanaendelea eneo hilo.

Kwa zaidi ya miaka saba, shule za msitu wa Boni zimekuwa zikifungwa kila mara na kulazimu watoto kubaki nyumbani na wazazi wao kutokana na utovu wa usalama ambao umekuwa ukichangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Bw Macharia aidha alishikilia kuwa msimamo wa serikali ni kuhakikisha maisha na shughuli za kawaida zinarejelewa msituni Boni, hivyo akawahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni ili wasome kama wengine nchini.

“Tumewasilisha walimu zaidi ya kumi kwenye shule za msitu wa Boni. Kila shule inahudumiwa na walimu wawili kwani wanafunzi wengi msituni Boni ni wa chekechea hadi darasa la nne. Tumeamuru shule zifunguliwe na tunashukuru kwani wanafunzi tayari wamefika shuleni kusoma. Usalama pia umedhibitiwa vilivyo kote Boni, ikizingatiwa kuwa serikali bado inaendeleza operesheni ya usalama eneo hilo. Wazazi na wanafunzi wasiwe na shaka,” akasema Bw Macharia.

Baadhi ya wazazi,walimu na wanafunzi waliozungumza na Taifa Leo hawakuficha furaha yao baada ya shule zao kufunguliwa.

Abdallah Wakati ambaye ni mzee wa jamii ya Waboni eneo la Kiangwe alisema ombi lake ni kuona shule za eneo hilo zikiendelea kuhudumu nyakati zote ili wanafunzi wao wasome na kuhitimu kama wengine.

Kijiji cha Kiangwe kilichoko msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu. Hatimaye watoto waliokuwa wakirandaranda vijijini eneo hilo warudi madarasani baada ya serikali kuzifungua shule sita. PICHA/KALUME KAZUNGU

“Kuna watoto wengi vijijini hapa ambao walianza kusoma zamani na walistahili wawe wamekamilisha masomo yao ya shule ya msingi. Hilo halijawezekana kutokana na kwamba shule zimekuwa zikifungwa mara kwa mara. Nafurahi kwamba hatimaye shule zetu zimefunguliwa japo kuchelewa. Ni matumaini yetu kwamba shule hizi zitaendelea kuhudumu ili wanafunzi wetu wabaki madarasani kusoma hadi wahitimu kama wengine nchini,” akasema Bw Wakati.

Farida Kokane aliisisitizia serikali kuongeza idadi ya walimu wanaohudumia shule za msitu wa Boni kwani walimu kumi pekee hawatoshi.

Bi Kokane pia aliiomba serikali kuboresha miundomsingi kwenye baadhi ya shule ili wanafunzi wawe na mahali pazuri pa kusomea.

“Shule zetu hapa msituni Boni zina changamoto ya majengo na mahali pa kukalia. Madarasa yako na nyufa zinazoficha nyoka. Pia madarasa hayana milango, ambapo wanyama wa msituni wamekuwa wakitafuta makao madarasani.  Serikali irekebishe hali duni ya shule zetu wakati inapozifungua,” akasema Bi Kokane.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa shule hizo, Diwani wa Basuba, Barissa Deko alishikilia kuwa ipo haja ya serikali kuanzisha kituo cha pamoja cha elimu eneo la Kiangwe ili kuhudumia wanafunzi kutoka vijiji vyote sita vya msitu wa Boni.

Alisema anaamini kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho kitakuwa cha bweni kutamaliza kabisa matatizo ya kielimu kwenye msitu wa Boni.

“Badala ya kila mara kufungua na kisha kufunga shule zetu, ni vyema kuanzishwe kituo cha pamoja cha elimu eneo la Kiangwe. Eneo hilo linafikika kwa urahisi ikilinganishwa na vijiji vingine eneo hili la msitu wa Boni. Walimu wa kutosha wapelekwe pale. Walinda usalama pia wasambazwe pale. Wanafunzi wawe wanasoma na kulala pale. Wakifanya hivyo sidhani watoto wa jamii yetu ya Waboni watahangaika kwa kukosa masomo kila mara kama ilivyo sasa,” akasema Bw Deko.

You can share this post!

Walinzi na wafuasi wa Bobi Wine wakamatwa, siku mbili kabla...

Mwanamume afa akiramba uroda lojing’i