• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Maraga awataka majaji kusimama kidete akistaafu

Maraga awataka majaji kusimama kidete akistaafu

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu anayestaafu, Bw David Maraga, amewataka majaji na mahakimu waendelee kusimama kidete katika utendakazi wao licha ya mawimbi makali yanayopiga Idara ya Mahakama nchini.

Akimkabidhi naibu wake, Jaji Philomena Mwilu, hatamu za uongozi wa asasi hiyo muhimu, Bw Maraga aliwashauri majaji waendelee kuwa watetezi thabiti wa Katiba na sheria.

“Nawahimiza muendelee kuwa thabiti katika utendakazi wenu, mkitetea Katiba na utawala wa sheria,” alisema.

Bw Maraga ni jaji mkuu wa pili kuongoza Idara ya Mahakama chini ya Katiba mpya ya 2010, baada ya mtangulizi wake Willy Mutunga.Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Bw Maraga alihudumu katika mahakama kwa miaka 18 kabla kuteuliwa kuongoza idara hiyo.

Katika hotuba yake ya mwisho jana, alipongeza majaji, mahakimu na kadhi kwa kuchapa kazi bila woga na kudumisha sheria na haki.Alisema idara hiyo ilikumbwa na mawimbi mengi lakini walistahimili yote.

Hususan, alitaja kukabiliwa na vitisho wakati mwingine huku idara ikinyimwa fedha na serikali ya kitaifa.Kufikia sasa Rais Uhuru Kenyatta amekataa kuwaapisha majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC).

“Nawahimiza mdumishe sheria katika utendakazi wenu. Muitetee Katiba na kuhakikisha haki imetendeka kila wakati ili wananchi waendelee kuwa na imani katika mahakama,” jaji huyo mkuu anayeondoka alishauri katika hafla ya kufana ya kustaafu kwake.Sherehe ya kumuaga ilitangulizwa na kikao maalum cha kusikiza ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kupitia kwa rais wake Nelson Havi.

Bw Havi aliwasilisha ombi la kumtaka Bw Maraga astaafu rasmi jana kisha jina lake liondolewe kwenye orodha ya majaji.Licha ya mivutano na Ofisi ya Rais, Bw Maraga aliipongeza pamoja na Bunge kwa kazi walizokamilisha pamoja.Alisema kwa muda huo wa miaka minne alioongoza mahakama alikamilisha kesi 172 na kufungua mahakama kuu mpya 22.

Isitoshe, aliajiri watumishi wa mahakama 194.Baada ya kukabidhiwa hatamu za kuwa Jaji Mkuu mwandamizi, Jaji Philomena Mwilu aliapa kuendeleza utendakazi bila woga wala upendeleo jinsi Bw Marafa alivyofanya.Jaji Mwilu alisema Idara ya Mahakama ilipata ufanisi mkuu chini ya uongozi wa bosi wake.

“Nikihudumu chini yako nimejifunza mengi, haswa uadilifu na uvumilifu,” akaeleza Jaji Mwilu.Alimtaka Bw Maraga asiwe na wasiwasi kwa vile kikosi cha majaji alichofanya kazi nacho kiko imara na kwamba watendeleza uongozi wa haki na ukweli.

Bi Mwilu alimsifu Bw Maraga kwa “kujitolea kwako mhanga kuleta ufanisi mkuu katika mahakama.”Alisema idara hiyo imekumbatia matumizi ya teknolojia chini ya uongozi wa Jaji Mkuu huyo anayeondoka.

Naye Bw Havi alimsifu Bw Maraga kwa “msimamo wake thabiti uliofanya mahakama nchini kuheshimiwa na asasi zote za serikali.”

Uamuzi mkubwa aliotoa Bw Maraga katika kipindi chake cha Jaji Mkuu ni kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais 2017 ambapo Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi.

You can share this post!

Raila atetea kuzungushwa kwa urais

Maraga asifiwa kwa kuongeza idadi ya korti nchini