• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Aliacha kazi ya udaktari kufuga nguruwe na kukuza migomba

Aliacha kazi ya udaktari kufuga nguruwe na kukuza migomba

Na SAMMY WAWERU

Ndoto yake akiwa mdogo kiumri ilikuwa awe rubani, ila ajali aliyohusika na kumuacha na majeraha mabaya ilibadilisha azimio hilo.

Jesse Ngugi alivunjika mkono wa kulia, mkono ambao kufikia sasa ungali na tatizo na kusalia na makovu. Ni mkasa uliogeuza matamanio yake, yakachukua mkondo wa taaluma tofauti.

Mwaka wa 2010, miaka miwili baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, Ngugi alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), kusomea kozi ya utabibu.

“Nilichagua taaluma ya masuala ya utabibu ili kuelewa kilichofanyika kwenye mkono wangu, na kutafiti kwa nini madaktari hawakuweza kuurekebisha kikamilifu,” anasema Dkt Ngugi.

Baada ya kufuzu, anasimulia kwamba alifanya mazoezi ya utabibu na kupata nafasi ya kazi katika hospitali moja kiungani nwa jiji la Nairobi.

Dkt Ngugi anasema tangu akiwa mdogo, alilelewa katika msingi wa kumcha Mungu, na alivutiwa sana na uimbaji. “Pindi tu baada ya kufanya KCSE, nilikuwa nimejiunga na taasisi moja nchini inayotoa mafunzo ya uanamuziki, nikasomea uchezaji gitaa na piano,” anafichua.

Mwaka wa 2016, alipungia kwaheri udaktari, akazamia uanamuziki na kuendeleza mafunzo, yalimnoa akawa msanii na produsa.

Hata hivyo, ndani yake alikuwa na wito uliomsumbua, wito wa kuingilia shughuli za kilimo. “Baba alitushawishi mara kwa mara tukumbatie kilimo-biashara, kutafuta mapato ya ziada,” anaelezea.

Anakotoka, Kijiji cha Irigiro, Saba Saba, Kaunti ya Murang’a ni tajika katika ukuzaji wa ndizi, ila wakulima wengi wakiwa wa zile asilia. Eneo hilo pia hukuzwa mahindi na maharagwe.

JKUAT ni maarufu katika masuala ya kilimo, na Ngugi alirejea humo kufanya utafiti mimea ambayo angekuza. Aidha, alishauriwa kulima ndizi zilizoimarishwa, tissue culture banana.

“Ndizi zilizoimarishwa ni rahisi kulima na zinachukua chini ya muda wa mwaka mmoja pekee kukomaa, kuanza kuvuna,” anasema David Muriuki, mtaalamu na afisa wa kilimo Kaunti ya Kirinyaga.

Isitoshe, mdau huyo anasema zina ustahimilivu wa hali ya juu kwa magonjwa na wadudu, huku mazao yakiwa ya kuridhisha.

Kulingana na Dkt Ngugi, shamba halikuwa kizingiti, na mwaka wa 2018 anasema aling’oa migomba yote ya ndizi asilia iliyopandwa awali, katika ekari moja na nusu.

Anafafanua, alipanda miche 761 ya tissue culture, kila mche akiuziwa Sh110 kutoka JKUAT. “Ni muhimu mkulima anunue miche kutoka kwa wazalishaji walioidhinishwa na Idara ya Kilimo ya Ukuzaji wa Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), ili kufanikisha ukuzaji wa ndizi zilizoimarishwa,” anashauri.

Kando na gharama ya miche, maandalizi ya shamba yalimgharimu Sh22, 830, mbolea Sh35, 000. Kimsingi, anasema mtaji jumla kuingilia ukuzaji wa tissue culture banana ulikuwa kima cha Sh141, 540, kupitia akiba yake na kiwango kingine akipigwa jeki na babak, kwa njia ya mkopo.

“Ufanisi katika kilimo unategemea kuwepo kwa maji ya kutosha, pembezoni mwa shambani langu kuna mto usiokauka, na ambao umechangia kustawisha jitihada zangu,” anasema mkulima huyo.

Miezi tisa baada ya upanzi, Ngugi anasema alivuna jumla ya kilo 5,159 za ndizi, akiuza kila kilo kati ya Sh12 – 15.

Licha ya kuwa anahisi alikandamizwa na mawakala, anaeleza kwamba aliridhishwa na mazao hayo.

Mawakala wanatajwa kama wafanyabiashara wahuni wanaovamia soko la mazao ya kilimo, kiasi cha kupunja wakulima, hata ikiwa wanasifiwa kufahamu waliko wanunuzi na wakulima, na kuondoa gharama ya usafirishaji wa bidhaa.

Dkt Ngugi anaendelea kufanya utafiti, na anaiambia Akilimali kwamba ameweza kuwaepuka kwa kujiivishia ndizi, ambapo huuzia wafanyabiashara mbalimbali masoko ya Murang’a, Kiambu na Nairobi.

Mazao yanapoongezwa thamani, bei huongezeka, na mkulima huyu anasema kilo moja ya ndizi zilizoiva haipungui Sh15.

Mazao yaliyopo shambani, anadokeza kwamba tayari amefanya mavuno ya tani 8, sawa na kilo 8, 000. “Kilo moja kwa sasa ni Sh18, na Februari 2021 ninatarajia kuvuna tani 4 zaidi,” anafichua.

Kwa sasa ana jumla ya ekari mbili anazolima ndizi zilizoimarishwa. Dkt Ngugi pia ni mfugaji hodari wa nguruwe, shughuli aliyoingilia Januari 2019. Ni ufugaji-biashara anaosema ulimgharimu mtaji wa Sh1.3 milioni kuuanzisha, kiwango kikubwa kikifadhiliwa na mapato ya ndizi.

Mradi huo, mapato makubwa yanatoka kupitia ujamiishaji na uzalishaji wa nguruwe, vivimbi akiwauzia wafugaji wenza, ambapo kufikia sasa anafichua ameuza zaidi ya 180, wenye umri wa miezi mitatu.

Mwana mmoja wa nguruwe hapungui Sh5, 000 huku anayeandaliwa kujamiishwa akimuuza zaidi ya Sh35, 000.

Isitoshe, ametia saini mkataba na Farmers Choice, kampuni tajika katika utengenezaji wa soseji.

Wakati wa mahojiano, Dkt Ngugi alisema tangu aingilie ufugaji wa nguruwe ameuza zaidi ya 150, makubaliano yake na Farmers Choice yakiwa Sh270 kwa kilo. Alisema kampuni hiyo hununua nguruwe mwenye uzani wa kati ya kilo 65 – 70.

Ni kilimo-ufugaji-biashara kinachoendelea kumtia tabasamu licha ya tatizo lake la mkono.

Alipoulizwa ikiwa anaweza kukiasi, alisema: “Mapato ninayopokea kupitia kilimo na ufugaji ni ya juu mno kuliko mshahara niliolipwa nikiwa daktari.”

 

You can share this post!

Ruto asukumwa ajiuzulu kwa kumkaidi Uhuru

FATAKI: Nani kasema mwanamke hana haki ya kukata kiu ya...