• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Mwilu mwanamke wa kwanza kuteuliwa kaimu Jaji Mkuu

Mwilu mwanamke wa kwanza kuteuliwa kaimu Jaji Mkuu

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa Jaji Mkuu Philomena Mbete Mwilu ndiye jaji mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi kuteuliwa kuwa kaimu Jaji Mkuu kuongoza idara ya mahakama.

Jaji Mwilu alikabidhiwa vyombo vya uongozi wa idara ya Mahakama na Jaji Mkuu David Maraga aliyestaafu Januari 11 2021 baada ya kuhitimu miaka 70.

Bw Maraga alimkabidhi Jaji Mwilu nakala ya Katiba ya Nchi hii, bendera ya idara ya mahakama na nakala ya kitabu kinachosimulia hali ilivyo mahakamani.

Jaji Mwilu aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu mwandamizi kwa mujibu wa kifungu nambari tano cha sheria za mahakama ambapo kinasema naibu wa Jaji Mkuu atahudumu kama Jaji Mkuu nafasi inapotokea aidha kutokana na kung’atuka kwake mamlakani ama kuaga..

Jaji Maraga alistaafu baada ya kuhudumia idara ya maiaka zaidi ya miaka 17.

Jaji maraga amkabidhi hatamu za uongozi naibu jaji Philomena Mwilu. Picha / Richard Munguti

Jaji Mwilu alikabidhiwa hatamu za uongozi wa idara ya mahakama katika hafla iliyofana sana katika jengo la Mahakama ya Juu. Jaji Mwilu sasa ndiye rais wa Mahakama ya Juu.

Atahudumu katika wadhifa huo wa Jaji Mkuu mwandamizi hadi tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama JSC itakapomteua Jaji Mkuu mpya kumrithi Bw Maraga aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miaka18.

Bw Maraga alianza hafla ya kustaafu kwake kwa maombi yaliyofanywa na viongozi wa kanisa la Sabato Pasta Dkt Blasious Ruguri.

Hata Oktoba 2016 wakati Jaji Maraga aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu Pasta Dkt Ruguri ndiye alimweka wakfu.

Jaji Mkuu David Maraga amkabidhi naibu wake Jaji Philomena Mbete Mwilu vyombo vya Jaji Mkuu mwandimizi. Picha/ Richard Munguti

Baada ya maombi Jaji Mwilu aliongoza kikao maalum cha mwisho ambapo Bw Maraga alikuwa miongoni mwa Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala na Isaac Lenaola.

Wakati wa kikao hicho rais wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Nelson Andayi Havi aliwasilisha ombi la jina la Jaji Mkuu Maraga liondolewe katika orodha la majaji kufuatia kustaafu kwake.

“Ombi lakubaliwa na jina la Jaji Maraga ambaye kufikia leo saa sita usiku atakuwa amestaafu limeondolewa katika majina ya majaji wanaohudumu nchini,” alisema Jaji Mwilu katika uamuzi wake.

Hafla hiyo haikuhudhuriwa na Jaji Njoki Ndung’u ambaye alikuwa na jambo rasmi alilokuwa anashughulikia.

Hata hivyo Jaji Mwilu alisema kwa vile majaji wa mahakama ya juu waliokuwako ni watano wanaweza sikiza kesi na kutoa uamuzi.

Baada ya kikao hicho cha mwisho na Jaji Maraga msafara wa majaji waliojumuisha rais wa mahakama ya rufaa Jaji William Ouko, Jaji Daniel Musinga , Jaji Martha Koome , Jaji Wanjiru Karanja, Jaji Milton Makhandia, Jaji Kathurima M’mntoinoti , Lydia Achode , Jaji Alfred Mabeya, Jaji Mumbi Ngugi na Jaji Prof Kariuki waliandamana hadi sembule ya Jaji mkuu ambapo hotuba za mwisho zilitolewa.

Wakati wa hafla hiyo ya kumuaga Jaji Mkuu (mstaafu) Maraga alitolewa nguo zake rasmi kisha akavaa nguo zake.

Pia gari lake rasmi na bendera yake Jaji Mkuu alizikabidhi msajili mkuu wa idara ya mahakama Bi Anne Amadi, Nguo rasmi alitolewa na aliyekuwa karani wake Bw Fidelis Simiyu.

Jaji Maraga alitandaziwa zulia nyekundu aliyotembelea akiwa ameandamana na mkewe hadi kwenye gari lao la kibnafsi iliyoendeshwa na afisa wa polisi.

Jaji Maraga aliwainulia mikono wote waliodhuria hafla hiyo na kuwapungia mkono wa buriani na kuwaaga akisema , “ Mungu awe nanyi daima.”

Nao wote waliinua mikono yao na kumuaga wakisema “ alitekeleza kazi yake kwa ukakamavu na ushujaa mwingi.

Jaji Maraga aliamua kesi 172 miongoni mwazo kesi ya uchaguzi wa urais wa 2017 ambapo aliwaongoza majaji wa mahakama ya juu kuharamisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Kesi hiyo iliwasilishwa na mwaniaji kiti cha urais wa chama cha ODM Raila Odinga.

Kufuatia kuharamishwa kwa ushindi wa Rais Kenyatta uhasama uliingia kati ya serikali kuu na idara ya mahakama.

Bajeti ya Mahakama ilipunguzwa na hata Rais Kenyatta akataa kuwaapisha majaji 41 wa mahakama za rufaa , leba na idara ya ardhi.

Ushauri wake wa mwisho kwa majaji na mahakimu ulikuwa watekeleze majukumu yao kwa ukakamavu na wawe stadi kusimamia na kuitetea katiba pamoja na kutenda haki.

Jaji Mwilu aliahidi kuendeleza haki na kuwa imara katika utenda kazi wake kabla ya kuteuliwa kwa mridhi wake.

“Unapoondoka usiwe na wasi wasi nitasimamia haki na ukweli kila wakati na kuhakikisha wananchi wamepata haki,” alisema Jaji Mwilu.

Jaji Mwilu alimlimbikizia sifa sufufu Bw Maraga na kumweleza kama jaji aliyesimama kidete bila kutingizika . Jaji Mwilu mwenye umri wa miaka 62 aliwahakikishia majaji na mahakimu kwamba atawaongoza katika kuendeleza kazi alizoacha Jaji Maraga.

Jaji Mwilu ndiye naibu wa jaji mkuu wa kwanza mwanamke kuhudumu kama Jaji Mkuu.

Manaibu wawili waliomtangulia Jaji Nancy Baraza na Jaji Kalpana Rawal waliohudumu chini ya Jaji Mkuu mstaafu Dkt Willy Mutunga walifurushwa.

Jaji Baraza alitimuliwa baada ya kumkung’uta pua bawabu katika maduka la Village Market. Jaji Rawal aliondolewa na mahakama ya juu baada ya kuhitimu umri wa miaka 70 licha ya kudai barua aliyoajiriwa nayo ilisema angelistaafu akihitimu umri wa miaka 74,

Jaji Rawal aliwakilishwa katika kesi hiyo na wakili mwenye tajriba ya juu Kioko Kilukumi. Kikao cha Mahakama ya Juu kilichoongozwa na Jaji Mutunga ndicho kilimtimua kazini.

Hata sasa Jaji Mwilu amewekewa viziki tele katika njia ya kuelekea kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke. Amewekewa kesi tatu katika JSC na nyingine katika mahakama kuu na mwanaharakati Okiya Omtatah.

Kesi hizo zinatokana na mkopo wa Sh60milioni aliochukua kutoka kwa benki ya Imperial iliyofilisika kisha akaulipa.

Katika tetezi zake Jaji Mwilu amesema kesi hizo zote zimewasilisha kwa lengo moja tu-kumzuia asiteuliwe kuwa Jaji Mkuu na JSC ilhali amehitimu.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Jikedume mambo yote’

Je, Ronaldo amefikia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote...