• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Je, Ronaldo amefikia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote duniani?

Je, Ronaldo amefikia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote duniani?

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo kwa sasa ni miongoni mwa wanasoka wanaoshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote duniani baada ya kupachika wavuni goli lake la 759 kitaaluma kwenye ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na waajiri wake Juventus dhidi ya Sassuolo mnamo Januari 11, 2021.

Akivalia jezi za Sporting Lisbon nchini Ureno, Ronaldo alipachika wavuni mabao matano kabla ya kufunga mengine 450 akiwa mchezaji wa Manchester United. Kabla ya kutua Juventus ambao kwa sasa amewafungia magoli 84, fowadi huyo alikuwa amewafungia Real Madrid magoli 450. Kufikia sasa, ametikisa nyavu za wapinzani mara 102 akiwajibikia timu yake ya taifa ya Ureno.

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu za mtandao wa Rec.Sport.Soccer Statistics Foundation (RSSSF), Josef Bican ndiye mfungaji bora wa muda wote (ukiondoa wachezaji ambao hawajawahi kucheza soka ya haiba kubwa) baada ya kufunga jumla ya mabao 805 kutokana na mechi 530.

Romario anafuata kwa mabao 772 akifuatwa na Pele aliyefunga magoli 767 katika enzi yake ya usogora.

Bican, ambaye aliaga dunia mnamo 2001, alichechezea vikosi vitano tofauti vikiwemo Rapid Vienna, Slavia Prague, Czechoslovakia na Austria kati ya 1931 na 1955.

Kati ya mabao hayo 805, alifunga 26 akivalia jezi za kikosi cha akiba cha Rapid huku akifunga baadhi ya mabao katika mechi zisizokuwa zimerasimishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Ukiondoa mabao hayo 26, ina maana kwamba Bican alikamilisha taaluma yake ya usogora akijivunia mabao 759 kutokana na mechi 495 kwa kuwa RSSSF inashikilia kwamba baadhi ya rekodi za jagina huyo alipokuwa akipiga soka ya kulipwa nchini Czech mnamo 1952 hazipatikani.

Ipo suitafahamu pia kwa rekodi za upande wa Pele na Romario baada ya wanasoka hao wawili raia wa Brazil kudai kwamba kila mmoja wao alifunga jumla ya mabao 1,000 walipokuwa wakitamba katika ulingo wa soka.

Lionel Messi wa Barcelona ndiye wa hivi majuzi kuvunja rekodi ya dunia ya Pele aliyefunga jumla ya mabao 643 akichezea klabu moja.

Hata hivyo, kikosi cha Santos nchini Brazil kilijitokeza na kudai kwamba Pele alifunga mabao mengi kutokana na mechi za kirafiki na magoli hayo hayakujumuishwa kwenye hesabu ya mabao ya nguli huyo ambaye kwa mujibu wao, aliwafungua jumla ya magoli 1,091.

Katika maelezo yake binafsi kwenye mtandao wa Instagram, Pele anadai kwamba ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa muda wote duniani kwa jumla ya mabao 1,283.

Hata hivyo, ukiondoa mabao kutokana na michuano kadhaa za kirafiki na mechi nyinginezo zisizokuwa rasmi ikiwemo ile aliyochezea timu ya taifa ya wanajeshi wa Brazil mnamo 1959, basi mabao rasmi ya Pele ni 757 ambayo alifunga akichezea Santos, New York Cosmos na timu ya taifa ya Brazil.

Romario alisherehekea bao lake la 1,000 mnamo 2007 japo idadi hiyo ya magoli inajumuisha pia yale aliyoyafunga akichezea vikosi vya chipukizi na akishiriki mechi za kirafiki na hisani.

Ingawa hivyo, mabao rasmi ya Romario yanakadiriwa kufikia 745 ambayo aliyafunga akivalia jezi za vikosi mbalimbali Australia, Asia, Bara Ulaya na Amerika Kusini.

Kwa hivyo, huenda Ronaldo ni miongoni mwa wafungaji bora wa muda wote duniani. Huenda. Pengine. Hakuna aliye na uhakika kwa kuwa hakuna rekodi bayana zinazoonyesha takwimu kamili za watangulizi wake.

Kilichoko wazi ni kwamba Messi kwa sasa amefungia Barcelona na timu ya taifa ya Argentina mabao 719 katika taaluma yake na ni pengo la magoli 40 linalotamalaki kati yake na Ronaldo.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwilu mwanamke wa kwanza kuteuliwa kaimu Jaji Mkuu

Sababu za Ozil kutaka kucheza soka ya kulipwa nchini...