Sababu za Ozil kutaka kucheza soka ya kulipwa nchini Amerika au Uturuki kabla ya kustaafu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Mesut Ozil wa Arsenal yuko katia hatua za mwisho za kuondoka ugani Emirates huku akihusishwa pakubwa na kikosi Fenerabahce nchini Uturuki au DC United kinachoshiriki kivumbi cha Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Kwa mujibu wa magazeti mengi ya Uingereza na Uturuki, Ozil anatarajiwa kutia saini kandarasi ya miaka mitatu na nusu na Fenerbahce ambao ni mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Uturuki (Turkish Super Lig).

Tetesi za Ozil kujiunga na Fenerbahce zilianzishwa na nyota huyo wa zamani wa Real Madrid ambaye alipakia kwenye mtandao wake wa Twitter picha yake mwenyewe akiwa jijini Istanbul. Chini ya picha hiyo, aliandika: “Huu mji…#throback #Istanbul.”

Ozil, 32, alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia timu ya taifa ya Ujerumani ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil baada ya kuwazidi nguvu Argentina.

Kwa mujibu wa gazeti la Fanatik nchini Uturuki, Ali Koc ambaye ni Mwenyekiti wa kikosi cha Fenerbahce alitua jijini London, Uingereza wiki jana kumshawishi Ozil ambaye ana usuli wa Uturuki, kujiunga na kikosi chake baada ya kuchipuka kwa ripoti kwamba kikosi cha DC United kilikuwa kimeanzisha mazungumzo na sogora huyo kwa nia ya kumsadikisha atue nchini Amerika.

Ozil alijiunga na Arsenal mnamo 2013 kwa kima cha Sh5.9 bilioni kutoka Real Madrid ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na wafalme mara 13 wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kufikia sasa, ndiye mwanasoka anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi (Sh49 milioni kwa wiki) katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na ndiye mwanasoka ghali zaidi katika historia ya Arsenal.

Iwapo atatua Fenerbahce, Ozil atakuwa akitia mfukoni kima cha Sh683 milioni pekee kwa mwaka. Fenerbahce, ambayo ni mojawapo ya klabu tatu kuu jijini Istanbul, kwa sasa inashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Turkish Super Lig.

Tangu aingie katika sajili rasmi ya Arsenal, Ozil amechangia mabao 54 katika kipindi cha miaka saba, 19 kati ya magoli hayo aliyochangia yakiwa katika msimu wa 2015-16. Alikuwa pia sehemu muhimu ya kikosi cha kocha Arsene Wenger kilichoshindia Arsenal mataji matatu ya Kombe la FA chini ya kipindi cha misimu minne.

Mchuano wake wa mwisho kambini mwa Arsenal ni mechi iliyoshuhudia kikosi cha Arteta kikisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya West Ham United mnamo Machi 7, 2020.

Ozil hakusajiliwa na Arsenal kwa minajili ya kampeni za msimu huu wa 2020-21 katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Europa League.

 “Kumekuwapo na changamoto tele. Lakini sijawahi kujutia maamuzi yangu ya kujiunga na Arsenal. Nimejivunia muda wangu kambini mwa kikosi hicho japo mambo yalibadilika ghafla baada ya mkurupuko wa janga la corona,” akatanguliza Ozil.

“Zipo nchi mbili ambazo ningependa sana kuchezea ligi zao kabla ya kustaafu ulingoni. Amerika na Uturuki. Iwapo ni Uturuki, basi timu nitakayoichezea ni Fenerbahce. Klabu hiyo ni sawa na Real Madrid ya Uhispania. Ndicho kikosi bora na kikubwa zaidi nchini humo,” akaongeza Ozil.

Miongoni mwa ofa ambazo Ozil amepewa na DC United ni idhini ya kupanua zaidi biashara yake ya mikahawa ya 39 ya Steps Coffe na M10 nchini Amerika kwa kufungua tawi jingine katika eneo la Audi Field linalomilikiwa na kikosi hicho jijini Washington DC.

Kubwa zaidi ambalo pia linatarajiwa kumshawishi nyota huyo wa zamani wa Real Madrid kutua Amerika ni uhusiano wa karibu kati ya wakala wake Erkut Sogut na Afisa Mkuu Mtendaji wa DC United, Sam Porter aliyehusika pakubwa katika kumsajili Wayne Rooney kutoka Everton mnamo 2018.

“Tuna kikosi kipana ambacho tunalenga kupunguza. Tunapania pia kushusha gharama yetu ya matumizi. Mengi ya mabadiliko tuliyoazimia kufanya kikosi mwishoni mwa msimu huu huenda yakaja mapema kwa sababu ya kupunguza gharama ya kukiendesha kikosi na kulipa wachezaji,” akasema kocha Mikel Arteta wa Arsenal kuhusu mipango ya vinara wa soka ugani Emirates mwezi huu wa Januari 2021.

“Ipo idadi kubwa ya wanasoka watakaoelekea kwingineko kwa mkopo huku baadhi wakitiwa mnadani. Hilo ndilo suala ambalo tumelipa kipaumbele kwa sababu kikosi kinapitia changamoto tele kwa upande wa fedha,” akaongeza kocha huyo raia wa Uhispania.

Japo Arsenal wamekuwa wakilenga kukatiza uhusiano na Ozil kwa muda mrefu uliopita, kiungo amekuwa akisisitiza haja ya kusalia ugani Emirates hadi mkataba wake utakapotamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa mtandao wa football.london, Ozil alikataa ofa ya kujiunga na kikosi kingine kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu kwa masharti kwamba Arsenal wangekuwa wakilipa asilimia 50 ya mshahara wake.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO