• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Pasta kusubiri Yesu korokoroni

Pasta kusubiri Yesu korokoroni

Na GEORGE MUNENE

PASTA wa dhehebu la Akorino aliyewanajisi na kuwatunga mimba binti zake wawili wenye umri wa chini ya miaka 18, sasa amefungwa jela kwa miaka 140. Pasta huyo wa miaka 51, anayetambulika kama John Gichira Gichini, alipatikana na hatia baada ya kukiri mashtaka.

Sasa ataishi gerezani maisha yake yote akisubiri kurudi kwa Yesu ambaye kwenye Biblia amehubiri habari za kurudi kwake siku ya kiama.

Katika uamuzi huo muhimu, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Baricho katika Kaunti ya Kirinyaga, Anthony Mwicigi alisema pasta huyo aliharibu maisha ya binti zake wawili, na hivyo alihitaji adhabu kali ili awe funzo kwa wengine.

Alimfafanua mzee huyo kama mtu mbaya sana, ambaye jina lake linapaswa kuingizwa katika sajili ya wahalifu sugu wa dhuluma za ngono nchini.

‘Mshukiwa alitumia vibaya nafasi yake kama baba na kuharibu maisha ya binti zake. Ni jambo la aibu na mwiko, na kwa sababu hiyo anahitaji kifungo cha muda mrefu gerezani,’ akasema hakimu kwenye uamuzi wake.

Akinukuu Biblia, Hakimu Mwicigi alisema pasta huyo alikuwa mtu mwovu ambaye siku zake za kuishi duniani zilikuwa zimehesabiwa.

‘Kumwogopa Mungu kunaongeza siku, lakini miaka ya watu waovu itafupishwa,’ alisema hakimu kuhusu makosa mawili dhidi ya pasta huyo ya kushiriki ngono na watoto wake ambapo alihukumiwa kuhudumu kifungo cha miaka 70 gerezani kwa kila moja.

Vifungo hivyo vitaambatana pamoja.Mnajisi huyo alikuwa ameshtakiwa kwamba kati ya Juni 2019 na Agosti 2020 aliwanajisi binti zake wenye umri wa miaka 14 na 16 katika eneobunge la Ndia.

Upande wa mashtaka ulieleza korti kwamba mhalifu hiyo anapaswa kutazamwa kama aliyepatikana na hatia kwa mara ya kwanza na kueleza kwamba vyeti vya ubatizo vya watoto hao viliashiria kwamba walikuwa wa chini ya umri wa miaka 18.

Fomu za P3 na nakala za matibabu zilizowasilishwa kortini kama ushahidi zilithibitisha kwamba watoto hao walidhulumiwa.

Akijitetea, Gichira alieleza korti kuwa ‘alipotoshwa na shetani’ kutenda makosa makubwa kama hayo, na kuomba msamaha kutoka kwa binti zake na mahakama.

Alisisitiza kwamba hakuna aliye mkamilifu kote duniani na hivyo anapaswa kuhurumiwa badala ya kulaaniwa.’Shetani bado hajafungwa. Bado anatawala duniani na kuwafanya watu kutenda dhambi.

Ni kweli nilitenda dhambi lakini ninajutia na nitafurahi sana ikiwa nitasamehewa. Ni mara yangu ya kwanza kutenda kosa kama hilo maishani mwangu,’ alijitetea.

Hakimu alieleza kwamba wasichana hao tayari wameacha shule baada ya kulemewa na ujauzito. Binti mkubwa tayari amejifungua.

Pasta huyo alikuwa akiwahadaa binti zake kuingia chumbani mwake wakati mama yao hakuwa nyumbani na kuwatishia kuwaua endapo wangefichua uovu aliokuwa akiwafanyia.

You can share this post!

Mshindi wa urais Uganda kujulikana kesho

Ruto azidisha uasi dhidi ya bosi wake