• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Uchaguzi wa Nairobi wasitishwa tena

Uchaguzi wa Nairobi wasitishwa tena

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Alhamisi imetoa agizo la pili la kusitisha uchaguzi mdogo wa Ugavana Nairobi kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bi Anne Kananu Mwenda aliyekuwa amependekezwa na gavana wa zamani Mike Sonko kuwa naibu wake Januari 6, 2020.

Jaji Antony Charo Mrima alitoa agizo hilo alipositisha kwa muda utekelezwaji wa Gazeti rasmi la Serikali nambari 10914 iliyotangaza tarehe ya uchaguzi mdogo wa Nairobi kuwa Feburuari 18,2021.

Wiki mbili zilizopita Jaji Mrima alisitisha kufanyika kwa uchaguzi huo mdogo kufuatia ombi la Bw Sonko kwamba utaratibu uliofuatwa na Bunge la Seneti kumtimua mamlakani ulikiuka sheria.

Hivyo basi Jaji Mrima alisitisha uchaguzi huo mdogo hadi wakati ule kesi aliyoshtaki Sonko itakaposikizwa na kuamuliwa.

Bi Mwenda naye aliwasilisha kesi nyingine akiomba mahakama isitishe uchaguzi huo mdogo kusubiri uamuzi wa bunge la kaunti ya Nairobi ikiwa itaidhinisha uteuzi wake kuwa naibu wa Gavana wa Nairobi na Bw Sonko mnamo Januari 6 2020.

Bi Kananu anasema katika kesi aliyowasilisha kuwa uteuzi wake kuwa naibu wa Gavana wa Nairobi ulikuwa halali.

“Hatua ya Bw Sonko kuniteua kuwa naibu wake mnamo Januari 6,2020 ilikuwa halali,” Bi Mwenda asema katika kesi aliyoshtaki mahakamani.

Pia anasema kesi iliyokuwa imewasilishwa na mpiga kura Bw Peter Odhiambo Agoro akipinga uteuzi wake na Sonko iliondolewa na hakuna kizingiti cha kumpinga asihojiwe na bunge la kaunti leo.

Lakini mwanaharakati Okiya Omtatah amewasilisha kesi akipinga bunge la kaunti ya Nairobi kuidhinisha uteuzi wa Kananu akisema “ Sonko hakuwa na mamlaka ya kumteua (kananu) kuwa naibu wake.”

Omtatah anasema Sonko anayekabiliwa na kesi tatu za ufisadi wa zaidi ya Sh350m hakuwa na mamlaka kisheria kumteua Kananu.

Anasema Jaji Mumbi Ngugi alikuwa amemzima Sonko kutekeleza majukumu yake ya ugavana hadi tatu za ufisadi dhidi yake ziamuliwe.

Omtatah anasema suala hili la ugavana limezua kizugumkuti kikali nchini na kwamba mahakama inapasa kuamua kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kananu na Sonko kabla ya bunge la kaunti ya Nairobi kumwidhinisha ndipo atwae hatamu za Gavana Nairobi.

You can share this post!

Ruto azidisha uasi dhidi ya bosi wake

BENSON MATHEKA: Wakenya wamechoshwa na undumakuwili wa...