• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Museveni kifua mbele Bobi Wine akipinga matokeo ya mapema

Museveni kifua mbele Bobi Wine akipinga matokeo ya mapema

 Na MASHIRIKA

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amepata uongozi wa mapema katika kinyang’anyiro cha urais, kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi Ijumaa, huku mpinzani wake Bobi Wine tayari akipinga matokeo hayo.

Kiongozi huyo mkongwe amepata kura 1,536,205 (sawa na asilimia 65.02) huku mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine akipata kuta 647,146 kutoka kwa vituo 8,310 ambazo kura zake zimekwisha kuhesabiwa.

Taifa la Uganda lina jumla ya vituo 34,684 vya kupigia kura. Bobi Wine tayari amedai kuwa kulikuwa na udanganyifu mwingi na fujo katika uchaguzi huo mkuu uliofanyika Alhamisi.

Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake. Vile vile, alidai kuwa baadhi ya maajenti wake walikamatwa na maafisa wa usalama

Lakini serikali ya Uganda imesema kuwa uchaguzi huo uliendeshwa katika mazingira ya amani na kwa njia huru na haki.

Mnamo Alhamisi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda (UEC) Simon Mugenyi Byabakama naye alitaja uchaguzi huo wa urais na ubunge kama uliofanikiwa zaidi.

Akiongea na wanahabari katika jiji kuu, Kampala, Bw Byabakama alisema kuwa wapiga kura walijitokeza kwa wingi na wakapiga kura kwa amani licha ya changamoto zilizosababishwa na janga la virusi vya corona.

Hata hivyo, kulishuhudiwa visa ambapo masanduku ya kupigia kura yaliwasili katika baadhi ya vituo kuchelewa. Vile vile, mitambo ya kuwatambua wapiga kura kieletroniki pia ilifeli katika baadhi ya vituo.

Lakini Bw Byabakama akitaja visa hivyo kama “vichache ambavyo athari zake ni finyu.”

Akihojiwa na kituo cha CNN Jumatatu, Rais Museveni ambaye ameongoza Uganda kwa miaka 35 tangu 1986, akisema ataondoka mamlakani ikiwa atashindwa “kwa njia ya haki.”

You can share this post!

Kananu aahidi kuunga mkono BBI

SAMMY WAWERU: Visa vya askari kujiua na kuangamiza wenzao...