Wakulima watakiwa kuwa wabunifu

Na SAMMY WAWERU

Wakulima na wafanyabiashara wametakiwa kukumbatia mfumo wa uongezaji mazao ya kilimo thamani ili kuyaepusha kuharibika.

Kwa upande wa wakulima, uongezaji thamani utawasaidia kukwepa kero la mawakala, mfumo huo ukisifiwa kufanya bei kuwa bora.

Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19 Machi 2020, wengi wa walioathirika waliingilia shughuli za kilimo, hatua hiyo ikiwa na maana kuwa kiwango cha mazao ya kilimo nchini kinaongezeka.

Masoko mengi nchini yanaendelea kushuhudia utupaji wa mazao hasa yasiyoweza kudumu muda mrefu.

“Wakulima na wafanyabiashara wakikumbatia mfumo wa uongezaji mazao ya kilimo thamani, utapunguza hasara hususan kwa yasiyodumu muda mrefu baada ya mavuno,” Jesse Ngugi, mkulima wa ndizi anaelezea.

Mkulima huyo huivisha ndizi badala ya kuziuza zikiwa mbichi, hatua ambayo anasema imechangia kuimarika kwa soko.

“Ndizi zilizoiva ni kati ya matunda yenye ushindani mkuu sokoni, kupata soko si kikwazo,” anasema, akiongeza kwamba anapania kuanza kutengeneza sharubati ya ndizi.

Isitoshe, Ngugi anasema kwa kukumbatia mfumo wa kuziongeza thamani ameweza kukwepa kero la mawakala.

Ukizuru masoko mengi nchini taswira itakayokulaki kwenye majaa yake ni ya mazao kama vile nyanya, machungwa, viazi, matikitimaji, vitunguu, mboga…yaliyotupwa kwa kukosa wanunuzi au kuashiria kuoza.

Mazao yaliyoathirika zaidi ni yanayodumu muda mfupi baada ya kuvunwa.

“Mboga zinaweza kuongezwa thamani kwa kuzikausha, zitumike wakati wa kiangazi au ukame,” anasema Paul Njeru, mkulima wa mbogamseto.

Anaendelea kufanya utafiti namna ya kuongeza thamani mboga anazolima, baada ya kuhangaika kupata soko la mazao yake amri ya kutoingia na kutotoka Kaunti ya Nairobi ilipokuwa ikitekelezwa 2020, kufuatia mlipuko wa virusi hatari vya corona.

Amri hiyo iliyotekelezwa kati ya Aprili na Julai kama njia mojawapo kuzuia kusambaza corona katika kaunti ambazo hazikuwa zimeandikisha maambukizi, iliathiri wakulima wengi hususan wanaotegemea masoko ya Nairobi na viunga vyake.

“Nilikadiria hasara kutokana na amri hiyo ndiposa nikaamua kutafiti jinsi ya kukausha mboga ili zitumike wakati wa kiangazi,” Njeru anaiambia Taifa Leo Dijitali.

Suala la mazao ya kilimo kuharibika kwa kukosa soko ni bayana katika masoko mengi nchini, na pia katika mashamba.

Wakulima na wafanyabiashara wakikumbatia mfumo wa kuyaongeza thamani, utawasaidia kwa kiwango kikubwa kuepuka hasara.

Mazao kama vile matunda ndiyo hutumika kuunda juisi na sharubati.

Habari zinazohusiana na hii