JAMVI: Uasi anaoshuhudia Rais ngomeni mwake si jambo geni

Na WANDERI KAMAU

UASI mkubwa wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa katika eneo la Mlima Kenya, umetajwa kuwa sawa na taswira iliyojitokeza katika maeneo ya Bonde la Ufa na Nyanza mnamo 2007 na 2013 mtawalia.

Wadadisi wanataja uasi huo kuwa “hali ya kawaida” wakati viongozi wakuu wa kisiasa katika maeneo fulani ya kisiasa wanapojitayarisha kung’atuka kutoka nafasi zao.Hadi sasa, Rais Uhuru Kenyatta hajamwidhinisha kiongozi yeyote kuchukua nafasi yake kama msemaji wa kisiasa wa ukanda huo, baada yake kustaafu kama rais mwaka ujao.

Katika eneo la Bonde la Ufa, Naibu Rais William Ruto aliongoza wimbi la ‘mapinduzi’ ya kisiasa dhidi ya chama cha Kanu na kupunguza ushawishi wa kisiasa wa marehemu Daniel Moi 2007.

Dkt Ruto alikuwa kwenye chama cha ODM pamoja na Bw Raila Odinga, aliyewania urais dhidi ya Rais Mstaafu Mwai KibakiDkt Ruto vile vile alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa ODM, kupitia kundi la ‘Pentagon’ lililowajumuisha yeye, Bw Odinga, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, marehemu Joe Nyaga na Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala.

Kulingana na wadadisi, sababu kuu ya ODM kupata umaarufu mkubwa katika eneo hilo ilitokana na hali kuwa wenyeji walihisi “kuchoshwa” na uongozi wa Bw Moi na Kanu.

“Uchaguzi wa 2007 ulishuhudia wimbi jipya la kisiasa katika Bonde la Ufa, hali iliyokuwa maasi ya wenyeji dhidi ya ushawishi wa Moi na Kanu. Huenda ndiyo taswira sawa inayoshuhudiwa Mlima Kenya,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

Kwenye ‘maasi’ hayo, wanawe Moi waliowania ubunge katika maeneo mbalimbali kwa tiketi ya Kanu pia walishindwa vibaya. Miongoni mwao ni marehemu Jonathan Toroitich, Raymond Moi na Seneta Gideon Moi.

Jonathan aliwania ubunge katika eneo la Eldama Ravine, Raymond katika eneo la Rongai (anakohudumu kama mbunge) na Gideon katika eneobunge la Baringo ya Kati.

Kwa mujibu wa Dkt Sang’, kuna uwezekano pia uasi huo ulichangiwa na uwepo wa kizazi kipya cha wapigakura, ambacho kilihisi Bw Moi hakuwakilisha maslahi yake hata kidogo.

“Tafiti zimeonyesha kuwa wale ambao waliunga mkono Kanu wakati huo walikuwa watu wenye umri uliosonga kidogo, kwani bado walimwanini Mzee Moi kama kiongozi wao na ishara ya umoja wa kisiasa,” akaeleza Dkt Sang.

Katika eneo la Nyanza, ODM ilipoteza viti kadhaa muhimu, hali iliyofasiriwa na wachanganuzi kama mwanzo wa “mwelekeo mpya kisiasa.’

Kivumbi kikali hasa kilijitokeza kwenye shughuli za mchujo katika uwaniaji ugavana katika Kaunti ya Siaya kati ya Bw William Oduor na Gavana Cornell Rasanga.Duru zilieleza kwamba vigogo wa ODM, akiwemo Bw Odinga, walimpendelea Bw Rasanga kupata tiketi ya chama hicho, huku idadi kubwa ya wenyeji wakimpendelea Bw Oduol.

Wadadisi wanasema ingawa hatimaye Bw Rasanga aliibuka mshindi, ni hali iliyoonyesha wananchi pia wanaweza kuamua mwelekeo mpya wa kisiasa wanaotaka kufuata, kando na hali inayoamuliwa na vigogo wakuu.Hilo ndilo pia linalotajwa kuendelea katika Mlima Kenya, wadadisi wakisema kuna uwezekano mkubwa wenyeji wameanza safari ya “mwelekeo mpya kisiasa” kinyume na hali ambayo imekuwepo.

Kwa mujibu wa Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa, hali hiyo ilidhihirishwa wazi na matokeo ya chaguzi ndogo za udiwani katika ukanda huo majuzi, ambapo Chama cha Jubilee (JP) kilishindwa vibaya na chama kipya cha People’s Empowerment Party (PEP) katika wadi za Gaturi (Murang’a) na London (Nakuru).

Wanasiasa kadhaa pia wamehama ama wanatazamia kuhama kutoka mrengo wa ‘Kieleweke’ ambao umekuwa ukimuunga mkono Rais Kenyatta na kupigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).Barua ya Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) kuhusu hali ya kisiasa ilivyo Mlima Kenya pia inarejelewa kuchora taswira kamili ya kisiasa kuhusu hali ilivyo.

“Hizi ni dalili za wazi kuwa kwa mara ya kwanza tangu uhuru, huenda eneo hili likafanya maamuzi yake kisiasa kwenye uchaguzi wa 2022 bila kuzingatia miito ama ushawishi wa viongozi wa kisiasa,” asema Prof Munene.

Kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa likitajwa kuwa “choyo” kisiasa, kwani huwa linasimama na kuwapigia kura wawaniaji wake pekee.Viongozi ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa humo ni Mzee Jomo Kenyatta, marehemu Stanley Matiba, Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Rais Kenyatta.

Kwa mujibu wa mbunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu) imefikia wakati wenyeji waanze kujifanyia maamuzi yao kisiasa, “kwani hivyo ndivyo watajikomboa kama maeneo mengine nchini.”

“Uchaguzi mkuu ujao utachora taswira tofauti sana katika eneo hili. Itakuwa mara ya kwanza kwa wenyeji kujifanyia maamuzi kwa njia huru bila kufuata upepo ama vishawishi vyovyote vya kisiasa,” akasema kwenye mahojiano.

Habari zinazohusiana na hii