Serikali yamrukia gavana kuhusu usalama

Na MARY WANGARI

SERIKALI imekanusha vikali madai ya Gavana wa Kaunti ya Mandera, Bw Ali Roba kuhusu hali ya usalama katika eneo la Kaskazini Mashariki ikionya kuwa matamshi ya kiongozi huyo yanaweza kuzidisha taharuki na kuhatarisha maisha ya Wakenya.

Kupitia taarifa kutoka Afisi ya Rais, Wizara ya Usalama wa Nchi jana ilipuuzilia mbali madai yaliyotolewa na Bw Roba mnamo Ijumaa, kuhusu jinsi wanamgambo wa Al-Shabaab wanavyozidi kuingia nchini na kudhibiti maeneo ya kaunti hiyo.

Kamishna wa Eneo la Kaskazini Mashariki Nicodemus Musyoki Ndalana, alifafanua kwamba Mandera ni miongoni mwa kaunti ambazo zimenufaika mno kutokana na hatua ya serikali kuwekeza pakubwa katika usalama nchini.

“Tumevutiwa na matamshi yaliyotolewa na Gavana wa Kaunti ya Mandera Ali Roba kwamba kundi la Al-Shabaab linazidi kuingia na kudhibiti maeneo ya ndani katika kaunti hiyo.

“Mandera ni miongoni mwa kaunti ambazo zimenufaika pakubwa kutokana na uwekezaji wa serikali kuu katika kuendeleza uimarishaji wa miundomsingi ya usalama, kutuma walinda usalama na kuboresha mifumo ya kukusanya habari,” alisema Bw Ndalana.

Alieleza kwamba serikali imejitolea kuendelea kubuni mikakati mipya katika juhudi za kuangamiza kero la ugaidi katika eneo hilo ambalo limekumbwa na misukosuko ya kiusalama.

Huku akikiri kwamba kaunti hiyo bado inakumbwa na visa vya kigaidi kutokana na eneo lake linalopakana na Somalia, serikali imesisitiza kwamba Kaunti ya Mandera si ngome ya magaidi tena.

“Kinyume na madai ya gavana, tangu 2013, Kaunti ya Mandera imepiga hatua kubwa kupitia vikosi vyetu vya usalama ambavyo vimekuwa vikikabiliana na kuzuia mashambulizi dhidi ya maisha ya wakazi na mali,” ilisema taarifa.

Kuhusu kurejelewa kwa masomo eneo hilo, Kamishna alisema kwamba shughuli za elimu zimeanza kwa kasi huku asilimia kubwa ya wanafunzi wakijitokeza licha ya upungufu wa walimu.

“Uwekezaji katika elimu umeimarika kwa kasi. Wasimamizi katika Serikali Kuu wametwikwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wote wamerejea shuleni huku idadi kubwa ya shule zikifunguliwa licha ya upungufu wa walimu na asilimia kubwa ya wanafunzi wakijitokeza,” alisema.

Kulingana na afisa huyo, serikali imekuwa ikishirikiana na kamati na mashirika mbalimbali kukusanya habari za kijasusi kutoka kwa raia ili kufanikisha jukumu lake la kulinda maisha na mali ya wananchi.

Haya yamejiri miaka miwili tangu kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab liliposhambulia hoteli ya Dusit D2 jijini Nairobi ambapo watu 22 waliuawa.