• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Wanafunzi wa elimu ya msingi waanza mitihani ya majaribio

Wanafunzi wa elimu ya msingi waanza mitihani ya majaribio

NA MARY WANGARI

WANAFUNZI wa Gredi ya Kwanza hadi Gredi ya Tatu na Darasa la Tano hadi la Saba wameanza mitihani ya majaribio yao ya Baraza la Mitihani Nchini (KNEC) hii leo Jumatatu, Januari 18, 2020, zoezi ambalo litakamilika hapo Ijumaa, Januari 22, 2020.

Mitihani hiyo ya Majaribio ya Maendelezo ya Elimu katika Elimu ya Msingi (LCBE) ni ya kwanza tangu shule zilipofunguliwa kote nchini mnamo Januari 4, kufuatia likizo ndefu ya zaidi ya miezi tisa kutokana na janga la Covid-19.

Kupitia taaarifa kutoka kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa KNEC, Mercy Karogo alisema kwamba majaribio hayo yatawawezesha walimu kugundua ni yapi wanafunzi walipoteza kielimu walipolazimika kukaa nyumbani kwa muda mrefu.

Aidha, Baraza hilo lilisema kwamba shughuli hiyo itawawezesha washikadau katika sekta ya elimu kubuni mikakati kabambe itakayowezesha kuimarisha elimu kwa kuzingatia nguvu na udhaifu wa wanafunzi.

“Lengo la majaribio haya kielimu ni kuwezesha kutambua mambo ambayo huenda tulipoteza kielimu wakati wa janga la Covid-19 na kupendekeza mikakati mwafaka ya kuziba nyufa hizo,” alisema bosi wa KNEC.

Wanafunzi wa Darasa la 7 watatahiniwa kwa masomo yote ikiwemo: Hisabati, Kiingereza, Kiwahili, Sayansi na Sayansi Jamii.

Wanafunzi wa Darasa la Tano na Darasa la Sita watatahiniwa katika masomo manne ambayo ni pamoja na Kiswahili, Kiingereza, Hisabati na Sayansi.

Kwa upande mwingine, wanafunzi wa Gredi One, Two na Three watajaribiwa kuhusu ujuzi wao wa maarifa na nambari kupitia shughuli za Hisabati, Kiswahili na Kiingereza, kulingana na KNEC.

Bosi huyo wa KNEC aliwahimiza wasimamizi wa shule na walimu kutilia maanani shughuli hiyo ya majaribio kwa kuhakikisha mazingira mwafaka kwa wanafunzi.

“Walimu wakuu na walimu wana wajibu muhimu wa kutekeleza ili matokeo ya majaribio hayo yawe ya kweli nay a kutegemewa,”

“Ninawahimiza kuhakikisha mazingira mwafaka kwa wanafunzi pasipo kutatizwa na masuala mengine yanayoweza kuathiri mat5okeo yao,” alisema.

Shughuli hiyo ya majaribio imeng’oa nanga huku wanafunzi wa Darasa la 8 wakizidii kujiandaa kwa mitihani yao kitaifa iliyopangiwa kuanza mnamo Machi mwaka huu.

You can share this post!

Messi apewa kadi nyekundu ya kwanza akichezea Barca

Sibabaishwi na matusi yenu, Uhuru awaambia Tangatanga