• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Fowadi matata Onyango atupwa nje ya timu ya taifa ya hoki

Fowadi matata Onyango atupwa nje ya timu ya taifa ya hoki

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Festus Onyango, 24, ametemwa kwenye timu ya taifa ya magongo itakayotegemewa na kocha Fidelis Kimanzi kwenye kampeni zijazo za kufuzu kwa Kombe la Afrika kuanzia Machi 2021 jijini Nairobi.

Kenya imetiwa katika zizi moja na Uganda, Tanzania, Burundi, Sudan, Libya na Ushelisheli katika mechi hizo zitakazoandaliwa katika uwanja wa Sikh Union.

Onyango ambaye ni mchezaji wa Butali Warriors alikuwa tegemeo la Kenya mnamo 2019 nchini Afrika Kusini kwenye kampeni za kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki za 2021 jijini Tokyo, Japan.

Katika mechi hizo, Onyango aliibuka mfungaji bora katika kikosi cha Kenya baada ya kupachika wavuni mabao manne. Nyota huyo ambaye ambaye ni nahodha wa zamani wa Strathmore Gladiators alikuwa na uhakika wa kuunga timu ya taifa ya hoki chini ya aliyekuwa mkufunzi wa kikosi hicho, Meshack Senge.

Katika msimu wa 2019, Onyango alitawazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Shirikisho la Hoki la Kenya (KHU) na akaibuka wa pili kwenye orodha ya wafungaji bora.

“Yasikitisha kwamba sikutiwa katika kikosi cha taifa. Kusema kweli, sijajua kiini cha kutemwa kwangu ila natakia kikosi kitakachowakilisha Kenya katika kampeni zijazo za kimataifa kila la heri,” akasema mchezaji huyo aliyeibuka mfungaji bora wa ligi mnamo 2017 baada ya kutikisa nyavu za wapinzani mara 20.

Mnamo 2018, Onyango alifunga jumla ya mabao 20, matatu nyuma ya George Mutira wa Butali Warriors aliyetawazwa Mfungaji Bora.

  • Tags

You can share this post!

KPA na Equity Bank kuwakilisha Kenya kwenye vikapu Afrika

Kiini cha wavulana kutorejea shuleni