• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
CECIL ODONGO: Heri wakubali, kumng’oa Ruto ni kibarua kigumu!

CECIL ODONGO: Heri wakubali, kumng’oa Ruto ni kibarua kigumu!

Na CECIL ODONGO?

SHINIKIZO za baadhi ya wanasiasa wa vyama vya ANC na ODM za kumtaka Naibu Rais Dkt William Ruto ajiuzulu au wamtimue bungeni ni za kujitafutia tu umaarufu wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2022.?

Mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula, ndiye anazidisha juhudi za kumtaka Dkt Ruto atimuliwe kwa upande wa ANC huku kiranja wa wachache Junet Mohammed na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo wakishinikiza hilo upande wa ODm.

Hoja kuu ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi hawa ni kwamba Dkt Ruto amemtaliki Rais Uhuru Kenyatta kisiasa na sasa anaikosoa serikali badala ya kuiunga mkono ikamilishe miradi yake kwa Wakenya.

Pia wanashikilia kwamba Dkt Ruto anaendeleza kampeni za uchaguzi wa 2022 na haungi mkono handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, ambayo wanasisitiza ndiyo itakuza umoja wa nchi.

Kwanza, wanasiasa hawa wanafaa wafahamu kwamba uwezekano wa Dkt Ruto kuondoka serikalini kabla ya 2022 ni finyu na huenda lisiwezekane kabisa.

Dkt Ruto ni mwanasiasa mweledi ambaye amekuwa akipanga karata yake ya kisiasa kwa makini na angekuwa ashaondoka serikalini angetaka kwa kuwa tayari uhusiano wake na Rais uliingia doa kitambo. Badala yake ameshatathmini athari au manufaa ya kujiondoa na akafanya uamuzi wa kutobanduka.

Pili, itakuwa vigumu sana kwa Rais Kenyatta kutoa baraka zake kwa wabunge wanaoegemea mrengo wake wamtimue Dkt Ruto kwa sababu kwa njia moja au nyingine itamwongezea Naibu Rais umaarufu wa kisiasa.

Tayari kauli mbiu ya kampeni zake maarufu kama Hustler Nation inaoana na Wakenya wa mapato ya chini hasa katika ngome zake, baadhi wakimwona kama mkombozi wao.

Aidha vyama vya ANC na ODM haviwezi kufikisha theluthi mbili ya wabunge wanaohitajika kikatiba kumbandua Dkt Ruto mamlakani. Kile Mabw Savula na Junet wanamakinikia zaidi ni kumsawiri Naibu Rais kama kiongozi ambaye hafai kuchaguliwa 2022 huku wakipigia debe Musalia Mudavadi na Raila Odinga.

Hata kama uhusiano wa Rais na Naibu wake si shwari tena sidhani kwamba Rais Kenyatta atawaamrisha majemedari wake wamtimue Dkt Ruto ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika kuchaguliwa kwake katika chaguzi za 2013 na 2017.

Kulingana na katiba ya sasa kumwondoa Naibu Rais afisini si rahisi kama chini ya katiba ya zamani ambapo Rais angemtimua makamu wake jinsi anavyotaka.

Kwa wakati moja Rais Daniel Moi alimtimua aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu George Saitoti na kudhihirisha mamlaka yake akamrejeshea wadhifa huo kupitia hotuba kwa umma akiwa kando ya barabara.

Katika historia ya taifa hili ni Jaramogi Oginga na Joseph Murumbi ambao walijiuzulu lakini hilo lilionekana kuwa pigo kubwa kwao kisiasa wakati huo wa utawala wa Kanu, mtindo ambao Dkt Ruto hataki kuufuata.

Wanasiasa wa ODM na ANC wakumbuke kwamba hata Bw Odinga hakujiondoa serikalini wakati ambapo alitofautiana vikali na Rais Mwai Kibaki katika serikali ya Muungano kati ya 2008-2013.

Badala yake ODM wanafaa wamvumishe Bw Odinga nao ANC Bw Mudavadi badala ya kujikita katika siasa za kumtaka tope Naibu Rais.? Kwa upande wake Dkt Ruto naye anafaa ajitokeze hadharani na atangaze kuwa ameanza rasmi kampeni za 2022 wala hamakinikii tena utekelezaji wa miradi ya serikali.

Kwa kulaumu handisheki kuwa ndiyo ilivuruga miradi ya serikali, ni kusema kwamba haungi mkono umoja wa nchi unaopigiwa debe na Rais Kenyatta.

You can share this post!

Majangili wazingira wabunge na wanahabari Kapedo

Maneno suka, shuka na zuka yana baidi kubwa kimaana