• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Serikali yaanza operesheni ya kuzima ujangili Kapedo

Serikali yaanza operesheni ya kuzima ujangili Kapedo

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imeanzisha operesheni kali katika eneo la Kapedo, kaunti ya Turkana kuwasaka majangili waliomuua afisa mmoja wa GSU.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisema kuwa kisa hicho kilitokea katika eneo la Amaya kati ya Kapedo na Chemolingot mwendo wa saa kumi na nusu jioni Jumapili.

“Inasikitisha kuwa maafisa wetu walishambuliwa na wahalifu hao wenye bunduki walipokuwa wakiendesha doria ya usalama katika eneo hilo. Emadau Temako ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa operesheni katika GSU aliuawa na wenzake wawili wanajeruhiwa,” Matiang’i akasema.

Waziri alieleza  kuwa maafisa hao walishambuliwa baada ya kufanyika kwa hafla ya kiapo iliyokuwa ikiendeshwa na wazee wa kitamaduni katika eneo hilo.

“Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa shambulio hilo lilitokea baada ya sherehe moja ya kiapo iliyoandaliwa na majangili,” Dkt Matiang’i akasema.

Waziri alisikitika kuwa maafisa wengi wa usalama wamepoteza maisha yao katika eneo hilo wakiwa kazini kurejesha amani akipata kwamba serikali haitapumzika hadi wahalifu hao watakaponaswa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Inspekta Jenerali wa Polisi ameanzisha operesheni katika eneo hilo kuwasaka majangili hao. Maafisa wa usalama watahakikisha wahusika wote wanakamatwa wakiwemo wazee waliokuwa wakiwalisha kiapo wauaji hao,” akasema Dkt Matiang’i kwenye taarifa.

Mnamo 2019 baada 21  waliuawa katika eneo hilo hilo la Kapedo katika operesheni ya kuimarisha usalama katika tukio la kusikitisha.

Kuhusiana na tukio la Jumapili, Waziri Matiang’i alielekeza kidole cha lawama kwa viongozi wa kisiasa katika eneo hilo kwa kuhujumu juhudi za serikali za kusaka suluhu la kudumu kwa mapigano ya kijamii katika eneo hilo.

You can share this post!

Maneno suka, shuka na zuka yana baidi kubwa kimaana

Mambo ya msingi kufahamu katika uandishi wa insha bora