Magara naye aongoza chama chake katika upande wake Ruto

Na VITALIS KIMUTAI

CHAMA cha People Democratic Party (PDP), kimemuunga Naibu Rais William Ruto siku chache baada ya aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto kuongoza Chama Cha Mashinani (CCM) kushirikiana naye.

Hatua hii inaendelea kuongeza umaarufu wa Dkt Ruto anayemezea urais huku Rais Uhuru Kenyatta akionekana kuwa na mipango ya kuzima azma yake.

“Kuna haja ya kubuni miungano kuleta pamoja vyama vya kisiasa, wanasiasa na wapigakura katika kundi la mahsla kabla ya uchaguzi mkuu. Ni kundi hili ambalo kwa hakika litashinda urais,” alisema kiongozi wa PDP, Bw Omingo Magara.

Alisema kwamba Dkt Ruto ndiye mgombeaji anayestahili kumrithi Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Bw Magara alisema kwamba kuna ujumbe wa wazi kutoka wa wapiga kura kote nchini kwamba hali ya uchumi ni mbaya na inafaa kurekebishwa kwa maono mapya yanayolenga kuimairisha maisha ya watu kuanzia mashinani.

Uhusiano wa Dkt Ruto na Bw Magara ni wa muda mrefu. Mnamo Septemba 22, 2007 wakiwa na wabunge Chris Obure na Chris Bichage walishambuliwa na vijana waliokuwa na hasira wakiwa Nyamarambe, Mugirango Kusini kuhudhuria harambee iliyoongozwa na aliyekuwa waziri wa fedha wakati huo Simeon Nyachae.

“Baada ya Bw Ruto kuongoza CCM kujiunga na kundi la mahsla, ni muhimu kwa Naibu Rais kufungulia milango kila mtu. Hatufai kufungia yeyote nchi tunapolenga kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alisema mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa.

Bw Ichung’wa alisema kuna wanasiasa wengi wanaosubiri kumuunga Dkt Ruto.“Lengo letu ni kuwasidia watu kote nchini na Ruto amejitolea kurekebisha uchumi na kuunganisha watu kustawisha nchi,” akasema.

BwIchung’wa.Dkt Ruto anapoendelea kupata uungwaji mkono, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju anapanga kuongoza maafisa wa chama hicho kuzima azima ya naibu rais ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Lakini washirika wa Dkt Ruto wanasema kwamba wamehama Jubilee.

“Tumehama Jubilee kabisa na hatutarudi. Wale ambao wanataka kutufukuza wanaweza kufanya hivyo,” alisema mbunge wa Belgut Nelson Koech.

Habari zinazohusiana na hii

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto