• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Maswali anayopaswa kujiuliza mwandishi yeyote wa kubuni kabla ya kuanza kutunga

Maswali anayopaswa kujiuliza mwandishi yeyote wa kubuni kabla ya kuanza kutunga

JUMA lililopita, nilionesha na kujadili jinsi mwandishi wa kubuni anaweza kupata visa vya kutungia hadithi.

Baadhi ya chemchemi za visa hivyo ni pamoja na ndoto, vyombo vya habari kama vile redio, runinga, magazeti, mtandao wa intaneti n.k, fasihi au tungo za waandishi wengine, tajriba za mwandishi au hata kuzungumza au kuwahoji wataalamu katika nyanja na taaluma nyingine.

Baada ya kupata kisa cha kutungia au kuandika kukihusu, mwandishi afanye nini? Hii ni hatua muhimu mno katika mchakato mzima wa uandishi wa kubuni.

Mwandishi anapaswa kujiuliza msururu wa maswali muhimu sana. Ni nini dhamira ya uandishi wangu? Maudhui ya utungo wangu ni yapi? Nitaisuka vipi hadithi yangu? Nitawasawiri vipi wahusika wangu?

Nitavipangaje vitushi katika hadithi yangu? Nitatumia nafsi gani katika usimulizi wa hadithi yangu? Itikadi ina dhima ipi katika usimulizi? Hadhira yangu ni ipi au ninawatungia kina nani?

Nitatunga katika utanzu gani?Haya, miongoni mwa maswali mengine yanawezka kumpa dira mwafaka mwandishi anayejitosa katika bahari na taaluma telezi ya uandishi wa kubuni.

Nimeyauliza maswali haya bila kufuata mpangilio wowote wala kuzingatia uzito wowote kwa sababu yote yana umuhimu sawa katika kufanikisha utunzi wa kubuni.

Aidha, katika makala ya awali, nilisema kuwa lugha ndiyo malighafi muhimu katika sanaa ya uandishi wa kubuni.Ninaamini kuwa mtu yeyote anayepania kujitosa katika ulingo wa kuandika fasihi lazima awe na umilisi mzuri wa lugha.

Umilisi wa lugha humsaidia mwandishi kuichezea lugha na kumfanya imtii katika uteuzi wa maneno ili kujenga taswira za kuvutia, kuaminika na kuvutia.

Uteuzi wa lugha

Mtunzi lazima atumie lugha itakayofikisha ujumbe unaokusudiwa. Lugha ya fasihi ni teule na maalum kwa minajili ya kuinata hadhira, kusisimua hisia za msomaji, kugusa nyoyo za wasomaji na kuathiri maono yao. Umuhimu wa lugha katika fasihi hujitokeza kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, lugha hutumiwa kuelezea maono ya mtunzi.

Kupitia kwa lugha, mwandishi anaweza kutoa fununu kuhusu falsafa na msimamo wake kuhusu suala fulani la jamii. Mwandishi Euphrase Kezilahabi huegemea mno itikadi ya udhanaishi (existentialism).

Katika takriban maandishi yake yote – Rosa Mistika, Kichwamaji, Dunia Uwanja wa Fujo, Gamba la Nyoka, Nagona na Mzingile – mtunzi huyu anaonekana akiuliza maswali ya kifalsafa: Maisha ni nini? Kifo ni nini? Mpaka kati ya kifo na uhai uko wapi? Raha ni nini? Je, Mungu yupo? Kezilahabi anauona mpaka baina ya maisha na kifo kuwa ni mwembamba mno – hivi kwamba, kuishi ni kufa.

Vilevile, Kezilahabi anayaona maisha kuwa ni adhabu na ya kukatisha tamaa. Takriban wahusika wakuu wote katika tungo zake zote huishia kufa kwa kujiua kwa sababu ya kukata tamaa.

Euphrase Kezilahabi hutumia lugha ya ‘kawaida’ na ‘nyepesi’ katika tungo zake zote.Katika riwaya ya Rosa Mistika, Kezilahabi anaonesha kwa uketo wa juu namna asasi za kijamii hasa familia na dini, shule (au mfumo mzima wa elimu) zimeshindwa kumlea binadamu. Rosa Mistika anaishia kujiua anapopata uhuru na kushindwa kuudhibiti. Eti uhuru pia una mipaka na hili hakulijua

[email protected]

You can share this post!

Magara naye aongoza chama chake katika upande wake Ruto

Muda uliosalia kabla ya mtihani wa kitaifa unatosha...