• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Ruto na Raila hawafai kupuuza agizo la Rais

Ruto na Raila hawafai kupuuza agizo la Rais

Na LEONARD ONYANGO

MNAMO Januari 3, mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa; viwanjani au kando ya barabara kwa kipindi cha siku 60.

Rais Kenyatta pia alipiga marufuku hafla za usiku na kuongeza muda wa kafyu hadi Machi 12, mwaka huu, huku akisema kuwa hatua hiyo ililenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Lakini inaonekana marufuku hiyo ya kufanya mikutano ya kisiasa ililenga tu Wakenya wengine na wala si wandani wa Rais Kenyatta.Siku 15 baada ya kutolewa kwa marufuku hiyo, tumeshuhudia mikutano tele ya kisiasa.

Naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamefanya mikutano kadhaa ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya nchi bila kizuizi kutoka kwa maafisa wa usalama. Badala yake viongozi hao wamekuwa wakipewa ulinzi na polisi wakati wa mikutano hiyo.

Baada ya kuhudhuria ibada wikendi iliyopita katika Kanisa la House of Hope mtaani Kayole, Nairobi, Naibu wa Rais Ruto aliyekuwa ameandamana na Askofu Margaret Wanjiru, walihutubia maelfu ya wafuasi kando ya barabara katika kile walichosema walikuwa wakiwajulia hali Wakenya walala hoi.

Ijumaa iliyopita, Naibu wa Rais alihutubia maelfu ya watu baada ya kuongoza hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya wahudumu 4,000 wa bodaboda na kutoa msaada wa mabasi kwa shule za upili za Kipsingei na Kapkelei katika eneo la Sotik, Kaunti ya Bomet.

Ni siku hiyo ambapo Naibu wa Rais na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto walitangaza kufanya kazi pamoja na kuzika uhasama wa kisiasa uliokuwepo baina yao katika kaburi la sahau.

Jumamosi, Naibu wa Rais aliyekuwa ameandamana na wabunge 40 – kwa mujibu wa ukurasa wake wa Facebook – alihutubia maelfu ya watu katika maeneo ya Kiserian na Matasia, Kaunti ya Kajiado.

Wiki iliyopita, Bw Odinga aliyekuwa ameandamana na mbunge Maalumu Maina Kamanda na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, walihutubia maelfu ya watu katika soko la Burma jiji Nairobi.

Kufikia sasa, wanasiasa hao hawajachukuliwa hatua yoyote kwa kukiuka agizo la rais na kuweka maisha ya wananchi katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Ikiwa Naibu wa Rais Ruto na Bw Odinga ambao ni wandani wa Rais Kenyatta wanakiuka maagizo ya kiongozi wa nchi, itawezekanaje kwa wananchi walala hoi wanaosaka tonge usiku na mchana kufuata masharti yaliyowekwa na wizara ya Afya kwa lengo la kupunguza maambukizi ya virusi vya corona?

Dkt Ruto na Bw Odinga wanafaa kuwa kielelezo kwa Wakenya.Hakuna haja ya kuzuia Wakenya maskini kujitafutia riziki usiku ilhali wanasiasa hawa wenye ushawishi wakikusanya watu kwenye mikutano ya kisiasa.

Ikiwa serikali imeshindwa kudhibiti wanasiasa hao, basi iondoe vikwazo vyote vilivyowekwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

Muda uliosalia kabla ya mtihani wa kitaifa unatosha...

WANTO WARUI: Huenda wanafunzi wengi wakakosa mitihani ya...