• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 1:25 PM
Kwa kila tone la mvua, wakazi wahofia usalama wao

Kwa kila tone la mvua, wakazi wahofia usalama wao

NA PAULINE ONGAJI

Ni picha inayonata macho pindi unapofika eneo la Shamakhokho kwenye makutano ya barabara za Serem na Hamisi. Nyumba ya kuta za matope na paa la mabati inayoning’inia kwenye ukingo wa korongo (gully).

Kila kuchao, korongo hii imezidi kuwa kubwa na kumeza sehemu ya mashamba ya wakazi watatu katika eneo hilo. Katika kipindi cha miaka michache, imeendelea kupanuka, kuongezeka kwa urefu na kina, suala ambalo limewaacha wakazi hawa na wasiwasi tele. Mmoja wa waathiriwa wakuu ni Wilson Lugano, 72.

Korongo hii imesababisha ufa mkubwa ambao umepasua na kumeza sehemu ya shamba lake, huku boma lake likionekana kana kwamba limeundwa kwenye ukingo wa vilima vya bonde la ufa.

Ni suala ambalo limemlazimu mwanawe, Fredrick Nyenze Boda, 45, kuhamia kwake na kuasi utamaduni wa jamii yake, usiomruhusu mwanamume mkomavu kuishi nyumba moja na baba mzazi.

“Nililazimika kuhamia nyumbani kwa babangu mita chache kutoka mahali ambapo nyumba yangu inaning’inia, kwani nilihofia huenda wakati mmoja mvua ikanyesha, kutufagia na kutuzika kwenye bonde hilo,” aeleza.

Mbali na suala la usalama, janga hili limesababisha hasara kubwa kwa familia hii. Mbali na mimea yao kufagiliwa kila mvua inaponyesha, kipande chao cha ardhi kilichosalia hakina faida kwao kamwe.

“Awali tulikuwa tunapanda aina mbalimbali ya mimea ikiwa ni pamoja na majani chai, ndizi na mahindi miongoni mwa mazao mengine yaliyokuwa yakituletea kipato. Lakini kwa sasa hilo haliwezekani kamwe kwani ufa huu umekuwa ukiendelea kupanuka, kurefuka na kuongezeka kwa kina kila kuchao,” alalama Lugano.

Mita chache kutoka shambani mwa Lugano, anaishi Eznah Khavere, mwanamke mlemavu wa umri wa makamo, ambaye ameendelea kuhesabu hasara kila kuchao kutokana na korongo hii.

“Kipande changu kikubwa cha ardhi kimemezwa na katika harakati hizo kuangamiza maelfu ya mimea yangu ya majani chai,” aeleza kupitia nduguye ,Timothy Ayodi.

Kwa Evans Shironye, mvua inaponyesha, maji kutoka barabarani hutirirka na kuingia kwenye kipande chao cha ardhi na katika harakati hizo kudhoofisha udongo. Sehemu hii imekuwa janga la usalama.

“Tuna bahati kwamba hakuna mtu ambaye amesombwa na maji na kufariki, lakini tunahofia kwamba huenda mambo yakawa mabaya siku za usoni,” aongeza. Anakumbuka wiki chache zilizopita ambapo kijana mmoja alianguka kwenye bonde la korongo hii alipokuwa anakimbizwa na polisi na kuvunjika miguu.

“Aidha, kuna wakati ng’ombe wetu alianguka na kuvunjika miguu. Ilitubidi kuingilia kwenye sehemu iliyo mbali na bonde hili ili kumvuta. Kwa bahati mbaya alikuwa amevunjika miguu na hivyo tulilazimika kumchinja,” asema Shironye, huku akiongeza kwamba wamelazimika kuzuia watoto wao kucheza karibu na eneo hili.

Pia, magari hayajasazwa. Kuna hatari ya magari yanayotumia barabara ya Shamakhokho- Senende kutumbukia kwenye shimo hilo ambalo limeendelea kutafuna sehemu ya barabara.V

ictor Mwanga anayeishi umbali wa mita chache kando yake, pia ni mwathiriwa wa janga hili. Sehemu ya shamba lake pia imemezwa na katika harakati hizo amepoteza mamia ya miti yake.Aidha, kiruko cha maji kilichokuwa shambani mwake, kimezibwa na udongo ambao umekuwa ukifagiliwa na maji ya mvua.

Kulingana na wakazi wa eneo hili, tatizo lilianza kama ufa mdogo uliosababishwa na mmomonyoko wa udongo kila maji ya mvua yalipokuwa yakitiririka kutoka barabara ya Shamakhokho –Hamisi na kumwagika hadi mashamba yao.

Lakini katika kipindi cha miaka michache, korongo hii imekuwa ikiongezeka kwa kina na tena upesi ambapo kwa sasa inakadiriwa kuwa na kipimo cha mita 15 kwa upana, futi 20 kwa kina, na zaidi ya mita 100 kwa urefu.Huku baadhi ya watu wakihoji kwamba huenda janga hili linatokana na wepesi wa aina ya udongo unaopatikana katika eneo la Vihiga, kwa wakazi, shida hii imetokana na ujenzi wa barabara.

Ujenzi wa barabara

Kulingana na Bw Mwanga ambaye pia ni mtaalamu wa kimazingira, tatizo lilianza katika miaka ya tisini, ujenzi wa barabara ya Shamakhokho- Seremi ulipoanza.

Mbali na kuathiri mandhari ya sehemu hii, kuna tatizo la mkondo wa maji ya mvua.“Mtaro wa kupitishia maji chini ya ardhi ulikuwa umejengwa kwenye kipande cha ardhi cha watu binafsi, ambapo muda ulivyokuwa ukisonga, mtaro huu uliziba na kuanza kutiririsha maji kwenye barabara ambayo ilikuwa imejengwa, kabla ya kuelekea katika mashamba ya watu binafsi,” anasema.

Kulingana na Dkt Jasper Omwenga, aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya kitaifa ya kudhibiti mazingira katika Kaunti ya Vihiga, kumekuwa na tatizo la mtiririsho wa maji katika eneo hili.Kulingana naye, maji yanayotiririka kando ya barabara hii yanapaswa kuvuja kidogo kidogo, lakini mambo sivyo.

Hapa, maji ya mvua yanatirika kwa zaidi ya kilomita mbili na kuteremka kupitia lango moja, suala ambalo laweza sababisha athari kubwa.

Hesbon Monda, mkurugenzi wa sasa wa Nema wa Kaunti ya Vihiga, anasema tatizo la mmnyonyoko wa udongo na korongo katika eneo hili limeangaziwa katika kamati ya mazingira ya kaunti.

“Hili ni janga kubwa la kimazingira, ni suala ambalo tumejadili na tunajaribu kupata suluhisho. Lakini ukweli ni kwamba ukarabati wa sehemu hii utahitaji rasilimali nyingi,” aongeza.

Ongezeko la mijengo

Mbali na hayo, Bw Mwanga anasema kwamba tatizo hili limekuwa baya zaidi kutokana na ongezeko la mijengo katika eneo hili.“Kuna ujenzi mwingi unaoendelea huku baadhi ya majumba yakiwa yamejengwa juu ya mitaro ya kupitisha maji chini ya ardhi. Aidha, hakuna mfumo uliowekwa ili kukinga maji ya mvua yanayotoka katika majengo haya,” anasema.

Lakini haya yakijiri, wakazi wanasema kwamba ngoja ngoja yao ya kupata suluhisho imeanza kwaumiza matumbo kwani imechukua muda mrefu.Kwa hivyo, katika harakati za kupunguza athari za janga hili, wamejaribu kubuni mbinu mbadala za kujaribu kuzuia korongo hii kuendelea kuzamisha mashamba yao.

Kwa mfano, wamepanda mamia ya mianzi kwenye ukingo wa korongo hii na hata kurusha baadhi ya miche ya mmea huu kwenye mabonde katika harakati za kuifanya ardhi kuwa thabiti, na hivyo kudhibiti mmonyoko wa udongo.

Japo kwa kiwango fulani jitihada zao zimezaa matunda, kila mvua inaponyesha, nguvu ya maji yanayotiririshwa kwenye mashamba yao, imeendelea kung’oa na kuzika mimea yao.

Na hivyo kwa kila tone la maji ya mvua, wakazi hawa wanaendelea kuhofia usalama sio tu wa rasilimali wanazomiliki, bali pia maisha yao.Lakini licha ya hatari hii, wanasema kwamba hawako tayari kuhama kwani hawana pa kwenda, huku wakitaka idara na mashirika husika kuingilia kati na kurejesha uzuri wa mazingira yao.

You can share this post!

MARY WANGARI: Kenya na Somalia zitafute njia ya kutatua...

Wakongwe wanavyoangamia wakimumunya raha ya dunia