• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kibarua cha kurejesha hadhi ya Amerika duniani chaanza

Kibarua cha kurejesha hadhi ya Amerika duniani chaanza

MASHIRIKA na SAMMY WAWERU

Ni bayana Bw Joe Biden ndiye Rais wa 46 wa Amerika, nchi yenye ushawishi mkubwa duniani, baada ya kuapishwa rasmi Januari 20, 2021.

Rais Biden na mgombea mwenza, Kamala Harris ambaye ni Makamu wake, aliibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Novemba 2020, ambapo alitoana kijasho na Bw Donald Trump ambaye kwa sasa ni ‘Rais Mstaafu’.

Katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 3, Rais Biden (Democrats) alizoa kura 290 za wajumbe dhidi ya 214 za Trump (Republican).

Licha ya kuwa Rais Trump amekubali kuondoka Ikulu ya White House, amekataa kukubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Uchaguzi wa urais Amerika, anayepata kura 270 wa kwanza huwa anatangazwa mshindi.

Msimamo wa Trump mwishoni mwa 2020 ulionekana kuchochea maandamano na ghasia katika miji ambayo ni ngome yake, huku wafuasi wa Rais Biden wakisherehekea.

Kichapo kingine kwa Bw Trump na ambaye utawala wake tangu 2016 alipomrithi Rais Mstaafu, Barrack Obama, ulizidi kukosolewa na wapinzani wake, ni pale bunge la seneti, Congres, lilipoidhinisha ushindi wa Rais Biden mnamo Januari 21, 2021 kwa kumchagua kwa kura 282, huku wabunge 138 wakipiga kura ya kupinga matokeo ya jimbo la Pennsyvania.

Ni shughuli iliyoendeshwa katika mazingira tata kufuatia uvamizi wa Capitol Hill na wafuasi wa Trump, ghasia zikizuka na kusababisha maafa ya watu kadha.

Chini ya utawala wa Rais Trump, nchi ya Amerika imeshuhudia mgawanyiko mkubwa, baina ya raia wenye rangi nyeupe na nyeusi.

Mgawanyiko huo ulikuwa wazi na bayana, hasa kufuatia mauaji ya kikatili ya George Floyd – Muamerika mweusi, mikononi mwa maafisa wa polisi.

Wakati wa kampeni za 2020 na baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, migawanyiko ilizidi kushuhudiwa.

Huku Rais Biden akichukua hatamu na mamlaka ya uongozi wa Amerika, ana kibarua kigumu kuhakikisha ameunganisha nchi hiyo.

Bw Trump akiondoka uongozini, ametajwa kama “Rais aliyepanda mbegu ya chuki kati ya raia wenye rangi nyeupe na nyeusi na kuleta mgawanyiko mkubwa”.

Chochezi zake alizozielekeza kwenye mitandao ya kijamii, zilikuwa zinalazimu Twitter na Facebook kuondoa baadhi ya jumbe na machapisho yake.

Aidha, baadhi ya vyombo vya habari Amerika pia vilikuwa vinasitisha ghafla hotuba ya Rais huyo, hasa anapoonekana kurusha cheche za maneno yanayotishia usalama wa kitaifa.

Bw Trump ametajwa kama rais aliyeacha rekodi mbaya ya uongozi katika historia ya utawala wa marais Amerika, haswa kutokana na tishio lake kutaka kukatalia mamlakani.

You can share this post!

Demokrasia imeshinda, asema Biden baada ya kuapishwa kuwa...

MWISHO WA GIZA!